Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KAMATI YAITAKA SERIKALI KUIWEZESHA NIT


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Selemani Kakoso ameelezea umuhimu wa Serikali kukiwezesha kikamilifu Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kiwe cha Kimataifa.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji ya Chuo hicho iliyowasilishwa katika kamati yake Mhe. Kakoso amesema NIT ni miongoni mwa vyuo vinavyofanya vizuri nchini hivyo kiwezeshwe kuwa na wataalam, watumishi  na vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunziaa ili kiweze kufikia malengo na kuimarisha sekta ya uchukuzi hapa nchini.

“Hakikisheni idadi ya watumishi inaongezwa ili wanafunzi wengi wa ndani na nje ya nchi wajiunge na Chuo hiki muhimu na hivyo kuliwezesha taifa kupata wataalam wa kutosha watakaosimamia  nyanja  zote za usafirishaji na uchukuzi nchini,” amesema Mwenyekiti Kakoso.

Aidha ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kukitangaza Chuo hicho na kukiwezesha kutoa kipaumbele katika kufundisha mafundi stadi na sanifu ili kuziba pengo lililopo kati na mafunzi stadi, sanifu na wahandisi nchini.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe.Atupele Mwakibete amesema Serikali ina mikakati ya dhati kuiwezesha NIT kuwa Chuo cha mfano kwa kuhakikisha kinatoa kozi zote zinazohusu usafiri wa ardhini, maji na anga na hivyo kuwawezesha wataalam watakaohudumu kwenye uwekezaji wa miradi ya  reli, meli, ndege na magari kupata stadi zao hapa nchini.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo ya Bunge imeitaka Sekta ya Uchukuzi kuhakikisha inasimamia kikamilifu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwenye eneo la mapato, tehama na masoko ili kuiwezesha bandari kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza mapato.

“Kukamilika kwa miradi ya upanuzi wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na kwenye Maziwa ya Tanganyika, Nyasa kutaongeza ufanisi wa bandari nchini’ amesisitiza Mwenyekiti Kakoso.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepitia taarifa ya utendaji kazi ya taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na kuhimiza ushirikiano miongoni mwa watumishi wa taasisi  ili kufikia malengo.