Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAIPONGEZA SERIKALI UWEKEZAJI SGR


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Seleman Kakoso, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR ambapo kwa sasa mradi huo unaendelea kutekelezwa kuanzia Dar es Salaam mpaka Mwanza yenye urefu wa kilomita takrbani 1,219.

Akizungumza jijini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Mwenyekiti Kakoso ameeleza kukamilika kwa mradi huo kutaongeza tija na ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kwa haraka na kwa wakati kutokea Bandari ya Dar es Salaam.

“Maamuzi ya kujenga reli ya SGR yalikuwa ya msingi sana ambapo tafiti zilizofanywa zimeonesha kuwa mradi huu utapunguza sana changamoto ya mzigo kucheleweshwa katika Bandari ya Dar es Salaam na utaongeza pato la Taifa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa zaidi ya nchi tano zinazotuzunguka zinategemea hasa bandari yetu”, amesema Mwenyekiti Kakoso.

Mwenyekiti Kakoso ameishauri Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kuhakikisha inawatumia vizuri wataalam walioshiriki kusimamia mradi huo toka awamu ya kwanza mpaka awamu ya tano inayoendelea ili kupunguza gharama kubwa za kuwarudisha wajenzi mradi utakapokamilika.

Aidha, Mwenyekiti Kakoso ameitaka Sekta ya Uchukuzi kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya sheria yanayopendekezwa kwa TAZARA ili kuifanya Mamlaka hiyo kuongeza tija na kujiendesha kwa faida.

Kwa upande wake Naibu Waziri Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema Serikali itaendelea kusimamia kila awamu ya ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kwa karibu ili uweze kukamilika kwa wakati kulingana na mkataba.

Mwakibete ameeleza kuwa pamoja na ujenzi huo Serikali inaendelea na manunuzi ya vitendea kazi mbalimbali ambapo inatarajiwa ndani ya mwezi Septemba na Oktoba kupokea mabehewa 22 mapya kwa reli ya kati na mabehewa 14 ya reli ya SGR ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya uendeshaji wa reli hiyo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepokea taarifa za utendaji wa TRC na TAZARA ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yake ya kuishauri Serikali na taasisi zake.