Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YASISITIZA VITENDEA KAZI MIRADI YA UJENZI NCHINI


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imelitaka Shirika la Reli Nchini (TRC),  kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wanaofanya kazi kwenye mradi wa reli ya kisasa ya SGR, Sehemu ya Mwanza hadi Isaka (km 341), wanapewa vitendea kazi na stahiki zao kwa kuzingatia miongozo ya ajira nchini.

 

Kauli hiyo imetolewa baada ya kamati hiyo kutembelea mradi huo na kubaini changamoto mbalimbali za kiutumishi kwa wafanyakazi hali inayoweza kupunguza morali ya wafanyakazi wa mradi huo.

 

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo  Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Seleman Kakoso, amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa utekelezaji wa mradi huo hivyo lazima wafanyakazi wafanye kazi kwa uzalendo kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

 

“Watumishi hawa ni watanzania na wanafanya kazi kwa uzalendo hivyo zingatieni taratibu zilizopo za ajira kwani kutowapa vifaa stahiki kwa ajili ya usalama wao inaweza kusababisha hujuma na Serikali ikashindwa kufikia malengo”, amesititiza Mwenyekiti Kakoso.

 

Mwenyekiti Kakoso ameongelea umuhimu wa Serikali kumsimamia Mkandarasi ili kuhakikisiha mradi huo unakamilika kwa kuzingatia viwango na muda uliopangwa ili kuwezesha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam na kuelekea kanda ya Ziwa.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amemuhakikishia Mwenyekiti huyo kuwa jicho la Wizara liko karibu kuhakikisha changamoto zilizopo zinatafutiwa ufumbuzi na kuharakisha mradi kukamilika kwa viwango vilivyokubalika kwenye mkataba.

 

Naibu Waziri  Mwakibete ameongeza kuwa lengo la Serikali kwa mradi wa reli ya kisasa ni kuhakikisha usafirishaji unarahisishwa kwa abiria na mizigo hivyo Serikali imeendelea kutoa fedha kwa wakati ili kuepusha kuchelewesha mradi.

 

Naye, Mkurugenzi wa Miunbombinu wa TRC, Mhandisi Kataraiya Faustine ameieleza Kamati kuwa ili kupunguza changamoto za wafanyakazi Shirika limeunda kamati ndogo ambayo iko kazini kupita kwenye mradi huo ili kubaini changamoto zote na kuzitafutia ufumbuzi.

 

Awali akitoa taarifa, Meneja mradi wa SGR sehemu ya Mwanza-Isaka (km 341), Mhandisi Masanja Machibya, ameeeleza kuwa mradi umefikia asilimia nne na  kazi zinazoedelea kwa sasa ni kujenga tuta katika maeneo mbalimbali,  uzalishaji kokoto na ukamilishaji wa majengo na ofisi za Wakandarasi.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge iko mkoani Mwanza kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.