Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ERB YASISITIZWA KUENDELEA KUNOA WAHANDISI


Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imesisitizwa kuendelea kuwapa ujuzi  unaohitajika wahandisi nchini ili kusaidia katika kuendeleza ubunifu na uvumbuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu Tasnia hiyo.

Rai hiyo imetolewa leo Septemba 6, 2024 na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Rahma Kassim Ali wakati akifunga Maadhimisho ya 21 Siku ya Wahandisi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambayo yamebebwa na kauli mbiu “Kuandaa Nguvukazi ya Uhandisi katika zama za Akili Mnemba - Mafunzo na Kuimarisha Ujuzi wa Wataalam wa Kada ya Uhandisi”.

“Nimpongeze Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa katika kusimamia na kuendeleza Sekta ya Ujenzi na taaluma ya uhandisi kwa ujumla, juhudi hizi zimewezesha  katika kuhakikisha kuwa miundonbinu yetu inaendelezwa na kusimamiwa na wahandisi wa ndani”, amesema Waziri huyo.

Amepongeza juhudi za ERB za kuhakikisha ushiriki mkubwa wa Wahandisi na Makampuni ya Ushauri ya ndani katika miradi mikubwa pamoja na msisitizo wa kutoa fursa kwa wahandisi kwani inawajengea uwezo wahandisi wa ndani na kuhakikisha wahandisi nchini wako mstari wa mbele kushiriki katika maendeleo ya Taifa.

Aidha, Waziri Ali amefurahishwa na Bodi hiyo  kwa kulibeba suala la uhaba wa walimu wa Sayansi na kulitafutia ufumbuzi kwa kuhakikisha shule zinapata walimu wa masomo hayo  na kuhamasisha wanafunzi hususan wa kike kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uajenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour ameeleza kuwa Mkutano huo wa siku mbili umetoa maarifa na mikakati muhimu ambayo itasaidia kushughulikia changamoto zinazojitokeza  katika taaluma ya kihandisi.