Habari
DKT. POSSI ASISITIZA USHIRIKIANO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dkt Ally Possi amemtaka Mkuu wa Chuo wa Taifa cha Usafirishaji (NIT), kushirikiana na taasisi za Sekta ya Uchukuzi na Nishati zinazotekeleza miradi ya kimkakati ili kurahisisha uendeshaji wa miradi hiyo itakapokamilika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara chuoni hapo, Dkt Possi amesema kupitia uwepo wa kozi zinazolenga miradi mikubwa kutaokoa fedha nyingi ambazo zimekuwa zikitumika kupeleka wataalam nje ya nchi ili kupata ujuzi wa uendeshaji wa miradi.
“Kwa sekta ya usafirishaji Serikali inakitegemea sana chuo hiki kwani tayari imenunua ndege zaidi 12, inajenga reli, bandari na bomba la mafuta, maeneo yote yanahitaji wataalam, hivyo shirikianeni na taasisi hizo ili wataalam mnaozalisha watusaidie kwenye uendeshaji pindi miradi itakapokamilika’ Amesema Dkt Possi.
Dkt. Possi ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza chuoni hapo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 2 kwa ajili ya manunuzi ya ndege za mafunzo ili kuwajengea uwezo wanafunzi wanaosoma kozi za usafiri wa anga.
Amefafanua kuwa miradi yote ambayo inatekelezwa chuoni hapo izingatie thamani ya fedha kwani Serikali imewekeza fedha za kutosha ili kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zakaria Mganilwa amesema kwa sasa Chuo kinajiimarisha katika kozi za uhandisi wa ndege, uhandisi katika meli na reli, kozi za mawasiliano katika reli lengo likiwa kusimamia uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR inayoejngwa nchini.
Prof. Mganilwa ameongeza kuwa chuo kina mpango wa kufungua matawi katika Mkoa wa Dodoma na Lindi ampbapo kwa Dodoma watazalishwa wataalam wa reli na tawi la Lindi eneo la Kikwetu watapatikana wajenzi wa meli, mafundi wa meli na miudombinu ya bandari.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi yuko katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam ya kutembelea taasisi zilizo chini ya sekta hiyo ili kuona shughuli mbalimbali za kiutendaji na kujadili namna bora ya kupata suluhu ya chagamoto zinazowakabili.