Habari
CHAMA CHA MADEREVA WA SERIKALI CHATOA MSAADA VITI MWENDO

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Makatibu Wakuu wa Wizara zote kuhakikisha wanaongeza ushiriki wa madereva wa Serikali katika Kongamano lao la kila mwaka ili kuongeza ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Bashungwa ameeleza hayo jijini Dodoma leo Agosti 27, 2024 wakati akipokea msaada wa viti mwendo 20 vilivyotolewa na Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum waliopo Shuleni.
“Nitoe wito kwa Makatibu Wakuu kutilia maanani hitaji la madereva kukutana kila mwaka kwasababu kongamano hizo wanajadili namna ya kuendelea kuongeza ufanisi na kubadilishana uzoefu”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amewataka madereva wa Serikali kuzingatia uadilifu na miiko ya taaluma ya udereva ili kuhakikisha usalama wa magari ya Serikali pamoja na watumiaji wengine na kuwa kioo kwa madereva wengine hata wa Sekta Binafsi.
Ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa madereva wa Serikali kupitia Chama cha Madereva Serikalini Tanzania (CMST), ili kukiimarisha, kukipa nguvu na hivyo kuendelea kusimamia vyema maslahi ya madereva Serikalini.
Akikabidhi Viti Mwendo, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Serikalini (CMST), Bi. Flora Mnyandavile ameeleza kuwa Chama hicho kimekabidhi viti 20 ambapo viti 5 vimekabidhiwa kwa ajili ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (Mb), viti 5 kwa ajili ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ambaye ni Mlezi wa Madereva, viti 5 kwa ajili ya Waziri wa Ujenzi, Mawasilino na Uchukuzi ya Serikali ya Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed (Mb) pamoja na vilivyobaki vitakabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi, Dkt. Charles Msonde amemhakikisha Waziri Bashungwa kuwa zawadi zilizopokelewa zitafikishwa kwa walengwa mapema kama ilivyokusudiwa.