Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BILIONI 2.55 ZATENGWA KWA AJILI YA MICHORO YA USALAMA BARABARANI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 2.55 kwa ajili ya uwekaji wa alama na michoro ya usalama barabarani kwenye Barabara Kuu na zile za Mikoa.

Hayo yameelezwa leo tarehe 30 Agosti, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri huyo wakati akijibu Swali la Mbunge Viti Maalum, Mheshimiwa Latifa Khamis Juakali, aliyehoji Serikali imejipangaje kufanya maboresho ya alama za barabarani?

“Katika mwaka wa fedha 2024/25 Wizara kupitia TANROADS imetenga Bilioni 2.55 kwa ajili ya uwekaji wa alama na michoro ya usalama barabarani, ikiwemo uwekaji wa alama za watu wenye mahitaji maalum katika mikoa yote 26”, amesema Kasekenya.

Kasekenya ameongeza kuwa kwa sasa Tanzania ina jumla ya alama 183 zinazotumiwa kwa ajili ya usalama barabarani na alama 180 kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum ambazo zinazotumika na nchi za Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika hatua nyingine, Eng. Kasekenya ameeleza kuwa Serikali inatarajia kusaini mkataba kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Nyang’hwale - Nyangho’longo – Nyambula (Kahama) ifikapo mwezi Septemba, 2024.

Aidha, Kasekenya amebainisha kuwa Serikali inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Nyang’hwale Jct (Busisi) – Wing3 – Nyang’wale – Nyangholongo – Nyambula (Kahama) (km 204.13) sehemu ya Busisi Ngoma – Wing3 yenye urefu wa kilometa 55.