Habari
BILIONI 11.4 KUJENGA DARAJA LA SUKUMA NA BARABARA UNGANISHI KM 2.2
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshatoa Shilingi Bilioni 11.4 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye mita 70 lililopo wilayani Magu mkoani Mwanza pamoja na barabara unganishi yenye kilometa 2.294
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 17 wilayani Magu mkoani Mwanza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa daraja hilo kati ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na kampuni ya Mkandaradi Mzawa ya Mumangi Construction Ltd.
“Jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan zinaonekana na ametuwezesha kiasi cha Shilingi Bilioni 11. 4 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili na babaraba unganishi zenye urefu wa kilometa 2.294, baada ya miezi 18 kama mkataba unavyotaka barabara na daraja vitakuwa vimeimalika na kutuepusha na ajali ambazo zingeweza kutokea” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amesema Serikali kupitia Wizara ya ujenzi itahakikisha Makandarasi wazawa wanapewa kazi na kuwasimamiwa ili waweze kufanya kazi hizo kwa kwa kiwango kinachotakiwa.
“Mkandarasi nakupongeza kwa namna unavyofanya kazi nzuri, hata nilivyokuwa Mkoa wa Mara niliona unapongezwa, nimekuja hapa wilayani Magu naona unapongezwa, mnanipa nguvu na mnampa nguvu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameelekeza Wizara ya Ujenzi kuandaa mpango mkakati kwa ajili ya makandarasi wazawa, nyie mmekuwa mfano kwa makandarasi wengine wazawa.” amesema Bashungwa
Kadhalika, Waziri Bashungwa amempongeza Mtendaji wa Tanroads, Mohamed Besta kwa kufanya kazi nzuri katika Mkoa wa Mwanza na kumuagiza afanye hivyo hivyo katika mikoa mingine.
“Niwatake mameneja wote wa TANROADS mfanye kazi kwa kushirikiana na viongozi, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wabunge kwa sababu wote tunajenga nchi yetu na ni nyumba moja lazima tushirikiane na tushirikishane kwa pamoja” amesema Bashungwa.
Vilevile, Waziri Bashungwa, ametoa wito kwa waendeshaji wa vyombo vya moto kuwa makini kwenye safari zao hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Naye, Mtendaji wa Tanroads, Mohamed Besta, amesema kuwa usanifu wa kina wa Daraja la Sukuma na barabara unganishi ulifanywa mwaka 2021/22 na kampuni ya kizalendo ya hapa nchini.
“Ujenzi wa daraja hili pamoja na barabara unganishi utazingatia matakwa ya kimkataba na muda wa ujenzi wa miuondombinu hii ni miezi 18” amesema Mhandisi Besta.
Kadhalika, amemhakikishia Waziri Bashungwa kwamba atasimamia vizuri ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara zake unganishi na kukamilika kwa muda uliopangwa na kusema kuwa litajengwa na makandarasi wa ndani.