Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BEHEWA MPYA ZAIDI YA 20 KUWASILI NCHINI SEPTEMBA


Serikali imesema mabehewa mapya ya abiria zaidi ya 20 ya reli ya kati yanatarajiwa kuwasili mapema mwezi Septemba mwaka huu kutokea Nchini Korea Kusini lengo likiwa kupunguza changamoto ya upungufu uliopo wa mabehewa  hususani kwa njia ya Mpanda na Kigoma.

Akizungumza Mkoani Kigoma Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema pamoja na mabehewa hayo mapya Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inafanya ukarabati mabehewa mengine takribani 30 ya abiria  na mabehewa mengine takribani 600 ya mizigo ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya Serikali  kuhakikisha mzigo mkubwa unasafirishwa kwa njia ya reli ili kunusuru fedha nyingi zinazotengwa kukarabati miundombinu ya barabara nchini.

“Serikali inaendelea na utekelezaji wa mpango wake wa kufanya maboresho makubwa kwenye miundombinu ya reli ikiwemo kuongeza mabehewa ya abiria na mizigo, nina imani mabehewa hayo yakiwasili changamoto ya upungufu wa mabehewa itakuwa imepata ufumbuzi amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameitaka TRC kupunguza urasimu kwenye upangaji wa mabehewa ya mizigo ili kuvutia wateja wengi zaidi hasa  wanaosafirisha bidhaa mbalimbali kupitia Bandari ya Kigoma na kuelekea Nchi Jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ester Mahawe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu hususani reli kwani kuboreshwa kwake kutainua uchumi wa Mkoa na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwa mikoa inayozunguka Ziwa Tanganyika na nchi Jirani.

Kwa upande wake Mratibu wa matengenezo ya njia na Mkuu wa Kitengo cha Usalama na Ulinzi wa reli  Mhandisi Ntejo Emmanuel amesema tayari TRC imejiandaa kupokea mabehewa hayo na kipaumbele kitakuwa kwa mikoa yenye idadi kubwa ya abiria na mizigo.

Mhandisi Emmanuel ameongeza kuwa kwa sasa TRC inakamilisha taratibu za manunuzi  za kumpata mkandarasi atakafanya maboresho kwenye vituo vya reli na njia kwenye sehemu ya Kaliua hadi Mpanda na Tabora hadi Kigoma ili kuhakikisha walaji wanapata bidhaa kwa wakati.

Naibu Waziri Mwakibete yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya siku tatu kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na kusimamiwa na Sekta ya Uchukuzi.