Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AZIDI KUTANGAZA NEEMA KWA MAKANDARASI WAZAWA, ASISITIZA UZALENDO


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka makandarasi wazawa kubadilika kifikra, kimtizamo, kuwa wazalendo na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili Serikali iendeleee kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa ya kutekeleza itakayowawezesha kukua.

Akizungumza na wakazi wa Tarakea wilayani Rombo mkoni Kilimanjaro, Waziri Bashungwa amesema Serikali imejipanga kuweka lami barabara ya Holili - Tarakea (km 51), ambapo tayari imeanza na sehemu ya mita 580 na itaendelea kujenga kwa lami km 10 sehemu ambayo haihitaji fidia ili kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo.

"Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwapa miradi mingi na mikubwa Makandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo wa kitaalam na kiuchumi, hivyo kuweni wazalendo na kamilisheni miradi kwa wakati na ubora", amesema Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa amemtaka Mkandarasi wa ndani M/s JP TRADERS LTD kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo ifikapo Februari mwakani kulingana na mkataba.

"Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshatoa kibali cha kuongeza kilometa 10 za barabara kwenye ujenzi wa mita 580 unaoendelea ambalo halina fidia ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo", amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro Eng. Motta Kyando, kuhakikisha wakati ujenzi wa barabara unaendelea uende sambamba na ukarabati wa barabara ya mbadala ili wananchi wasiathirike kutokana na ujenzi huo.
Bashungwa amewahakishia wakazi wa Tarakea wilayani Rombo kwamba tayari usanifu wa barabara ya Elerai - Kamwanga (km 39), umekamilika na ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utaanza hivi karibuni ili kuboresha shughuli za utalii na kukuza uchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkandarasi M/s TRADERS LTD anayejenga sehemu ya mita 580 eneo la Nayemi njia panda ya Tarakea amemhakikishia Waziri wa Ujenzi kumaliza barabara hiyo kwa wakati na kujenga kwa kiwango cha lami kinachotakiwa ili  kujenga imani kwa Serikali na kuweza kuwaamini makandarasi wazawa kwa kuwapa miradi mingine.