Habari
BASHUNGWA AENDELEA KUPIGILIA MSUMARI SUALA LA MAKANDARASI WAZAWA
Waziri wa Ujenzi, innocent Bashungwa ameziagiza Bodi za Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kuhakikisha zinaandaa mpango kazi wa kusimamia na kuimarisha taaluma ya Sekta ya Ujenzi nchini ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wake ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia.
Bashungwa ameyasemaa hayo leo Tarehe 06 Novemba, 2023 jijini Dodoma, alipokuwa akizindua Bodi za ushauri za CRB na ERB ambazo zinaundwa kwa mujibu wa sheria ili kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Bodi hizo.
Amesema kuwa Takwimu zinaonyesha kuwa suala la upatikanaji wa fursa nchini katika utekelezaji wa miradi kwa makandarasi wa ndani haliridhishi kutokana na kuwa licha ya makandarasi wa ndani kuwa wengi bado miradi wanayoitekeleza ni michache ukilinganisha na makandarasi wa nje.
“Muandae mpango kazi wa kusaidia Makandarasi wa ndani, muujadili, kuutathmini na kuusimamia kwa pamoja badala ya kulalamika makandarasi wa ndani hawapati fursa”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema kuwa Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya makandarasi waliosajiliwa ni 14800 kati ya hao 14300 ni makandarasi wa ndani sawa na asilimi 54 na 500 ni makandarasi wa Nje sawa na asilimia 46, huku ukija kwenye suala la upatikanaji wa keki ya Taifa, makandarasi wa nje wanafaidi kuliko wa ndani.
Pia, Bashungwa amesisitiza kwa bodi hizo kuongeza ushirikiano mzuri walionao ili kusaidia taaluma hiyo kufanya kazi vizuri na kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amesema kuwa Bodi ya Usajili Makandarasi (CRB) ina wajumbe wasiozidi nane ambao wameteuliwa na Waziri wa Ujenzi kwa kuzingatia vifungu vya sheria.
“Wajumbe hawa wanatoka Wizara ya Ujenzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi, Chama cha Wahandisi Washauri, Chama cha wabunifu Majengo, Chama cha wakandarasi pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara” amesema Balozi Aisha.
Halikadhalika, Balozi Amour amesema kuwa Bodi ya ERB inaundwa na wajumbe nane pamoja na Mwenyekiti mmoja.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga amemhakikishia Waziri Bashungwa kuwa watatekeleza dhamana waliopewa kwa uadilifu mkubwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya bodi kwa mujibu wa Sheria,Kanuni na Taratibu ili kuleta tija na ufanisi kwa Taasisi wanazozisimamia.