Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AAGIZA UKARABATI WA BARABARA ZA CHANGARAWE.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi Eng. Emil Zengo kuhakikisha anaiboresha barabara ya Kiranjeranje – Nanjilinji – Makangada kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika misimu yote ya mwaka.

Bashungwa ameeleza hayo leo Novemba 04, 2024 jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini aliyehoji Serikali imefikia hatua gani ya kuboresha barabara ya Kiranjeranje – Nanjilinji ili magari yanayochukua mizigo yaweze kupita katika mazingira mazuri?

“Nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 140 kwa ajili ya kurudisha miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mvua katika Mkoa wa Lindi na barabara hii ni miongoni mwa hizo zilizoathirika, Hivyo nimuelekeza Meneja wa TANROADS kuitembelea na kuhakikisha anaikarabati kwa kiwango cha changarawe kama Mbunge alivyoomba”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia TANROADS, imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nangurukuru – Kilwa Masoko yenye urefu wa kilometa 30 na kueleza kuwa Serikali imeweka kipaumbele kuboresha barabara hiyo ili iende sambamba na ukamilishaji wa Bandari ya Kilwa Masoko ili kuongeza tija.

Vilevile, Bashungwa amewaeleza Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali kupitia TANROADS kwa kushirikiana na TARURA imejipanga kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanakuwepo nyakati zote katika vipindi vya mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha hapa nchini.

Katika hatua nyingine, Bashungwa ameeleza Wizara ya Ujenzi itapitia maombi ya upandishwaji hadhi wa barabara ya Bashnet – Luqmanda – Bosedesh hadi Zinga kupitia Bodi ya Barabara ya Mkoa kuona kama barabara hiyo itakidhi vigezo vya upandishwaji hadhi kama ombi la Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Hanang.