Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA PUGE – ZIBA – CHOMA (TABORA) KUJENGWA KWA AWAMU: KASEKENYA


Serikali imepanga kuanza kwa awamu ujenzi wa barabara ya Puge – Ziba – Choma sehemu ya Puge – Ndala (km 5), Ziba – Choma (km 2) na Ziba – Nkinga (km 4) kwa kiwango cha lami Mkoani Tabora.

Hayo yameelezwa leo Novemba 06, 2024 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mheshimiwa Seif Gulamali, Mbunge wa jimbo la Manonga aliyehoji Je lini ujenzi wa barabara ya lami kutoka Choma – Ziba - Nkinga hadi Puge utaanza lini?

“Katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa kilometa 11 wa sehemu ya Puge – Ndala (km 5), Ziba – Choma (km 2) na Ziba – Nkinga (km 4) kwa kiwango cha lami”, amesema Eng. Kasekenya.

Aidha, Eng. Kasekenya ameeleza kuwa Serikali inategemea kutangaza zabuni ya kumpata Mkandarasi wa kuanza sehemu ya ujenzi wa barabara hiyo mwezi Novemba, 2024.

Katika hatua nyingine, Eng. Kasekenya amelihakikishia Bunge kuwa Wizara itaanza hivi karibuni ujenzi wa daraja la lukuledi ambalo ni moja kati ya madaraja yaliyoathiriwa na mvua za El – Nino na tayari limeingizwa katika utaratibu wa kulijenga upya kupitia fedha za dharura zilizotolewa na Benki ya Dunia.