Habari
BARABARA YA ‘FUFU’ (DODOMA - IRINGA) YAFUNGULIWA RASMI BAADA YA UKARABATI.

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imekamilisha ujenzi wa barabara ya Dodoma - Iringa eneo la Fufu kwa kunyanyua tuta la barabara lenye urefu wa kilomita 4 na kujenga makalvati makubwa manne uliogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 8.7.
Barabara hiyo imefunguliwa rasmi kuanza kutumika leo tarehe 16 Oktoba 2025 na Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo wa dharura umezingatia viwango vya ubora ili kuondoa changamoto iliyokuwepo hapo awali ya kujaa maji na kusababisha adha kwa wasafiri na wasafirishaji.
“Tumekamilisha ujenzi wa barabara ya kipande cha fufu kilichokuwa kinajaa sana maji, na makalvati yalikuwa madogo ambayo yalikuwa yanashindwa kupitisha maji na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara ambao walikuwa wanasubiri Kwa saa kadhaa ili waweze kupita”, ameeleza Mhandisi Zuhura.
Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa barabara hiyo imejengwa na Mkandarasi Mzawa kampuni ya GNSM Contractors Limited Kwa mkataba wa mwaka mmoja na mpaka sasa imekamilika kwa asilimia 97 na kazi zilizobakia ni uwekaji wa alama za barabarani pamoja na kingo za barabara.
Aidha, Mhandisi Zuhura ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya dharura ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 kiasi cha Shilingi Bilioni 35.6 zilitengwa.
Kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Fufu wameipongeza Serikali Kwa kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao utachochea biashara na pia wameomba kuwekewa kivuko cha kuvusha mifugo pamoja na kujenga mitaro ili kuruhusu maji yaweze kupita kwa urahisi, hadi kwenye Makalvati mapya yakiyojengwa na kutosababisha uharibu tena wa maji katika kijiji cha Geza Ulole.
Naye, Dereva wa magari makubwa anaetumia Barabara hiyo Bw. Juli Daudi ameishukuru Serikali kwa ukarabati wa barabara hiyo na kuondokana na adha ya kupita kwa muda mrefu katika barabara ya changarawe ya mchepuo ambapo walikuwa wakitumia dakika 35 hadi 40 na sasa hivi watatumia dakika 5 hadi 10.