Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ATCL NA TCAA ZAPONGEZWA


Serikali imetakiwa kuiwezesha Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), kwa kuiwekea mazingira rafiki ya kujiendesha kwa kuweka watendaji wenye mtazamo wa kibiashara.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Seleman Kakoso mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji ya kampuni hiyo na taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), ambapo pamoja na mambo mengine amezipongeza taasisi hizo kwa kazi nzuri wanazozifanya katika utoaji wa huduma bora kwa wadau na udhibiti wa usafiri wa anga nchini.

“Serikali wekezeni zaidi katika Kampuni ya ATCL ili iweze kufanya vizuri zaidi kibiashara na isaidieni kumaliza madeni yaliyokuwepo kipindi cha nyuma”, amesisitiza Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Kakoso.

Aidha, Kamati hiyo ya Miundombinu imezungumzia umuhimu wa Serikali kuendelea kusimamia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), katika uboreshaji wa viwanja vya ndege vinavyoendelea kujengwa ikiwemo vya Iringa na Musoma na kusisitiza kasi katika ujenzi wake.

“Simamieni kwa karibu ujenzi wa viwanja vya ndege hapa nchini ili kuiwezesha ATCL kufanya vizuri kwa kuwa ufanisi wa kampuni hiyo unahitaji ubora wa viwanja vya ndege nchini”, amefafanua Mhe. Kakoso.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, ameieleza Kamati hiyo kuwa ujenzi na uboreshaji wa baadhi ya viwanja vya ndege hapa nchini vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake na Serikali tayari imepata fedha za uboreshaji wa viwanja vya Ndege vya Tanga na Lindi.

Awali akitoa taarifa ya Utendaji wa Kampuni ya ATCL, Afisa Mtendaji Mkuu wa ATCL Eng. Ladislaus Matindi ameieleza Kamati hiyo kuwa Kampuni imefanikiwa kufanya ushirikiano wa kibiashara na makampuni saba (7), ya ndege ambayo ni Qatar Airways, Air India, Emirates, KLM, Omani Air, Rwanda Air na Ethiopian Airlines ambapo mashirikiano hayo yamelenga kuhakikisha muungano wa safari kwa abiria wa ATCL na mashirika hayo katika maeneo ambayo ATCL itakuwa haifanyi safari zake.

Ameongeza kuwa Kampuni hiyo imeongeza vituo na kufanya mtandao wa safari wa ATCL kufikia vituo 26 ambapo vituo 15 vya ndani na tisa (9) ni vya nje.

Amevitaja vituo hivyo kuwa ni Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Mbeya, Mpanda, Mwanza, Mtwara, Songea, Tabora na Zanzibar wakati vya nje ni Bujumbura, Entebbe, Hahaya, Harare, Lusaka, Ndola, Nairobi, Johannesburg na Lubumbashi na vituo viwili (2) ni vya nje ya Afrika nchi ambavyo ni Mumbai - India na Guangzhuo - China.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Hamza Johari, ameileza Kamati hiyo kuwa Mamlaka imefanikiwa kusaini upya mkataba ya usafiri wa anga kati yake na nchi nyingine ili kufungua soko la usafiri wa anga kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa anga, kuvutia mashirika mengine kutoa huduma nchini na kuimarisha ushindani katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.

Hamza ameongeza kuwa Mamlaka imefanikiwa kutoa leseni mpya 1,223 na kuhuisha leseni 270 katika fani mbalimbali katika Sekta ya usafiri wa anga.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imepokea, kujadili na kushauri taarifa ya utendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).