Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Adhabu kali kutolewa kwa wasafirishaji wanaokiuka sheria - RC Andengenye


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Thobias Andengenye amesema kuwa adhabu kali zitatolewa kwa wasafirishaji wanaokiuka Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari pamoja na makosa tofauti yanayohusisha huduma za mizani.

Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika kwa siku moja mkoani humo.

“Anaezidisha uzito anaweza pia akasababisha ajali, hii inaweza ikapelekea akafungiwa shughuli za usafirishaji kwa muda au hata kufungiwa moja kwa moja. Adhabu tofauti na uzidishaji uzito wa magari ni faini ya Dola za Kimarekani 15,000 au kifungo cha miaka mitatu. Adhabu hiyo pia itahusisha watumishi wa mizani wanaokula njama na wasafirishaji ambao sio waaminifu.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi mahiri wa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuwekeza katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya barabara nchini yaani barabara kuu, barabara za mikoa pamoja na barabara za mijini na vijijini, lengo likiwa ni kuharakisha kasi ya maendeleo ya Taifa letu”, amesema Andengenye.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Esther Mahawe, ameipongeza Serikali, kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara nchini na kuwataka wadau wa usafirishaji kushiriki kikamilifu katika jitihada za Serikali za kuleta maendeleo nchini.

Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma alimuambia Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari kwa wadau wa usafirishaji ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa miundombinu ya barabara nchini, na kuhakikisha kuwa zinadumu kwa muda uliokusudiwa.

Kwa upande wake msimamizi wa Mizani kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Leonard Saukwa amewaambia waandishi wa habari kuwa, adhabu zitokanazo na uzidishaji uzito wa magari zinatofautiana kulingana na uzito unaozidishwa kwenye gari husika.

“Hata hivyo, yapo makosa ambayo wadau wa usafirishaji wanayatenda mara kwa mara tofauti na uzidishaji uzito katika magari, na wanapokiri makosa hayo basi wasafirishaji hao hutozwa faini ya dola za Kimarekani 2,000” amesema Mhandisi Saukwa.

Nao wadau wa usafirishaji wanaohudhuria mafunzo hayo mkoani Kigoma, wamesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa wao kudhibiti uzito wa magari yao kwa kubeba mzigo isiyozidi uzito, na hivyo kuepusha uharibifu wa mara kwa mara wa magari yao lakini pia kuepusha uharibifu wa barabara ambazo Serikali inatumia fedha nyingi kuzijenga pamoja na kuzikarabati.

Semina ya mafunzo kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inahusisha wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, madereva, pamoja na wadau wengine wa usafirishaji kutoka Serikalini pamoja na sekta binafsi.