Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ABIRIA KIWANJA CHA NDEGE SONGWE WAONGEZEKA


Abiria wanaotumia Kiwanja cha Ndege cha Songwe wameripotiwa kuongezeka kutoka abiria elfu sitini na tisa (69,000) kwa mwaka 2020/2021 hadi elfu themanini na tano (85,000) kwa mwaka 2021/22 ikiwa ni matokeo ya upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songwe.

Akizungumza jijni Mbeya mara baada ya kukagua upanuzi wa Kiwanja hicho pamoja na Wabunge wa Mkoa huo Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema kukamilika kwa mradi huo kumefanya kiwanja hicho kufanya kazi kwa saa 24 na hivyo kurahisisha zaidi shughuli za usafirishaji baina ya mkoa huo na mikoa mingine nchini.

“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye upanuzi wa kiwanja hiki ambapo baadhi ya maeneo ujenzi umekamilika na maeneo mengine kazi zinaendelea kwa kasi”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema nia ya Serikali ni kuongeza miudombinu rafiki na wezeshi kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo mbalimbali ikiwemo bidhaa za mbogamboga na matunda zinazozalishwa katika mikoa ya nyanda za juu kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.

Naye Mbunge wa Mbeya Vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Mbeya, Oran Njeza amesema kuwa kiwanja hicho kuwa na miudombinu ya kisasa na uwezo wa kufanya kazi saa ishirini na nne ni fursa kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani kuongeza kipato kwani biashara zitafanyika wakati wote.

Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Mhandisi Danstan Komba,  amesema kwa sasa mradi wa kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua, taa na uzio umekamilika kwa asilimia mia moja na ujenzi wa jengo la abiria unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Songwe umehusisha kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege kutoka mita 3000 hadi mita 3330, taa, uzio na jengo la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500 kwa wakati mmoja.