Habari
WIZARA YA UJENZI, TANROADS WAJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NINO TABORA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imejipanga kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha nchini.
Dkt. Msonde ameyasema hayo leo Septemba 28, 2026 wakati akikagua maendeleo ya Ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo tofauti, wilaya ya Kaliua na Urambo Mkoani Tabora, ambapo amezipongeza juhudi zinazofanywa na TANROADS Mkoa wa Tabora katika kuimarisha madaraja, makalvati na maeneo mengine korofi yanayoweza kuathiriwa na mvua kubwa.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha miundombinu ya barabara na madaraja inaendelea kuwa salama na kupitika wakati wa msimu wa mvua.
“Nimefurahi kufika katika Daraja la Mwongozo hapa Kaliua, na kuona kuwa limejengwa kwa uimara na kutanuliwa. Kabla ya hapo daraja hili lilikuwa dogo na maji yalikuwa yakipita juu ya daraja. Tunaamini sasa hata mvua zikiwa nyingi hazitaweza kuleta athari hapa,” amesema Dkt. Msonde.
Aidha, Dkt. Msonde amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora, Mhandisi Mlimaji, kuendelea kuwasimamia makandarasi wanaotekeleza kazi za matengenezo ya barabara na madaraja, ili kuhakikisha kazi hizo zinakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Sambamba na hilo, Dkt. Msonde amepongeza juhudi zinazofanywa na TANROADS Mkoa wa Tabora katika kuendelea kukarabati barabara ya Tabora Mjini–Ulyankulu yenye urefu wa kilomita 90, kwa lengo la kuhakikisha inaendelea kupitika kipindi chote cha mwaka wakati taratibu za ujenzi wake kwa kiwango cha lami zikiendelea.
Ameeleza kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa Mkoa wa Tabora na mikoa jirani ya Shinyanga na Katavi, hivyo kuwa na umuhimu katika kurahisisha usafiri na usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji amesema, usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa barabara ya Tabora–Ulyankulu yenye urefu wa kilomita 90, ipo katika hatua za mwisho na kwa sasa imefikia asilimia 97 ya utekelezaji wake.
