Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAZIRI ULEGA AKABIDHIWA OFISI NA WAZIRI BASHUNGWA, WIZARA YA UJENZI.


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya uteuzi na mabadiliko ya Viongozi, Disemba 08, 2024.

Makabidhiano hayo yamefanyika, leo Disemba 16, 2024 katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi zilizopo Mtumba Mkoani Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine Waziri Bashungwa amempongeza Waziri Ulega na kumusisitiza kuendelea kusimamia utekekelezaji wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Ujenzi.

Akizungumza na watumishi, Waziri Bashungwa amewashukuru kwa ushirikiano aliyoupata kutoka kwa Menejimenti na Watumishi wa Wizara ya Ujenzi na kusisitiza ushirikiano huo pia kumpatia Waziri Ulega ili kuendekea kulisukuma gurudumu la maendeleo kupitia Sekta hiyo.

“Watumishi na Wataalam hawa ni wachapakazi, wanajituma usiku na mchana hata katika kile kipindi cha Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya kilivyoathiri miundombinu ya barabara na madaraja, wataalam hawa walihakikisha wanarudisha mawasiliano kwa wakati”, amesema Bashungwa.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumteua kusimamia Sekta ya Ujenzi na kumuahidi Mheshimiwa Rais kuendelea kutekeleza pale alipoishia mtangulizi wake.

Ulega ameomba ushirikiano kwa Menejimenti na Watumishi wa Wizara hiyo ili kukidhi mahitaji ya wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuwajengea miundombinu bora na ya uhakika.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu Balozi Mhandisi Aisha Amour, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Charles Msonde, Menejimenti pamoja na watumishi wa Wizara ya Ujenzi.