Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAZIRI MBARAWA AMKABIDHI OFISI WAZIRI BASHUNGWA


Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amezungumzia umuhimu wa Wizara ya Ujenzi kuendeleza miradi ya kimkakakati ya ujenzi wa barabara kwa utaratibu wa uhandisi, manunuzi ujenzi na fedha (EPC+F) na ujenzi wa miradi kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP) ili kufikia matarajio ya Serikali.

Akizungumza wakati akimkabidhi Ofisi Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, jijini Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kazi kubwa ya kuweka misingi ya kuendeleza miradi hiyo imekamilika hivyo kazi iliyobaki ni kuendelea na kasi ya uendelezaji wa miradi hiyo.

“Mheshimiwa Waziri unayo timu nzuri ya kukusaidia kufanya kazi, hivyo itumie na kuwaongezea uzoefu wa kimataifa katika kusimamia miradi ili kuiwezesha Tanzania kuendana na kasi ya mabadiliko ya miundombinu ya kidunia”, amesisitiza Profesa Mbarawa.

Amezungumzia umuhimu wa Wizara kujenga uwezo wa kutayarisha wahandisi washauri wa miradi inayotekelezwa nchini badala ya kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi kama ilivyo sasa.

Aidha, Profesa Mbarawa amewashukuru wataalamu na watumishi wa Wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano waliompa na kumsisitiza Waziri Bashungwa kuendeleza ushirikiano huo ili kufanikisha malengo ya Sekta.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa,  amemshukuru Profesa Mbarawa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kutekeleza miradi mikubwa ya barabara, madaraja, nyumba na ujenzi wa wa viwanja vya ndege na kuahidi kuendeleza utamaduni huo ili kuleta tija kwa wananchi.

“Tutahakikisha msingi uliojenga tunauendeleza hususan kuongeza barabara za kisasa, nyumba za viongozi na watumishi wa umma na kuhakikisha vivivuko na utengenezaji wa magari unakuwa wa uhakika”, amesema Waziri Bashungwa.

Katibu Mkuu, Mha. Balozi Aisha Amour, amemshukuru Profesa Mbarawa kwa miongozo yake na kumuahidi kumpa ushirikiano Mheshiwa Bashungwa katika usimamizi wa miradi mbalimbali ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya Sita katika uendelezaji wa miundombinu nchini.

Mheshimiwa Bashungwa leo amekabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Mbarawa mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 30, 2023 kuwa Waziri wa Ujenzi kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu wakuu.