Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WAZIRI BASHUNGWA: MAKANDARASI WABABAISHAJI KUCHUKULIWA HATUA.


Serikali imetoa onyo kali dhidi ya Makandarasi wababaishaji na kusisitiza hatua kali za kisheria kuchukuliwa kwa mkandarasi yeyote atakayekiuka miiko na maadili ya taaluma yake.

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, wilayani Mpwapwa jijini Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kipande cha Mbande - Kongwa Junction - Ng'ambi - Mpwapwa (km 5).

Aidha, Bashungwa amewaagiza Mameneja wa TANROADS katika mikoa yote nchini kuhakikisha kila mwezi wanaandaa orodha ya Makandarasi wababaishaji na kutuma Wizarani ili hatua stahiki dhidi yao kuchukuliwa mapema.

"Sitegemei kuona kuna Wakandarasi wababaishaji katika miradi ya TANROADS, ikibainika kuwepo kwa baadhi yao hakikisha Meneja unamchukulia hatua kali za kisheria kwa mujibu wa mkataba sitaki kuona hali ya Misenyi inajitokeza kwenye miradi ya TANROADS",  amesema Bashungwa.

Amesisitiza kuzipima Bodi za Usajili wa wahandisi (ERB) na Bodi za Usajili wa Makandarsi (CRB) kwa kuhakikisha wanafuatilia miradi yote ambayo inasuasua na kuchukua hatua katika miradi hiyo.

Halikadhalika kuhusu ujenzi wa barabara ya  Mbande - Kongwa -  Junction - Mpwapwa sehemu ya Kongwa Mpwapwa  (Km 32) kwa kiwango cha lami, Waziri Bashungwa amesema kuwa Mkandarasi ameshapatikana na muda si mrefu serikali itasaini mkataba na ujenzi kuanza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Colman Gaston amesema kuwa ujenzi wa barabara sehemu ya Kongwa - Mpwapwa (km 32)  inatarajiwa kujengwa na mkandarasi  M/ S Estim Construction ambapo maandalizi ya kutia saini mkataba wa ujenzi yanaendelea.

Naye, Mbunge wa Mpwapwa, Mhe. George Malima amesema kuwa imani ya wananchi wake ni kupata barabara ya lami na kusisitiza kuwa ni matarajio yake kuwa ahadi hiyo itatimia kwani imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wilaya kongwe kama hiyo kukosa barabara ya lami.

"Wilaya hii ni kongwe ilianza tangu mwaka 1926 tunashangaa hadi leo haina barabara ya lami, tunaamini kuja kwako kutakuwa mkombozi katika wilaya hii", amesema  Malima.