Habari
WAZIRI BASHUNGWA AMBANA MKANDARASI CHICO, UCHELEWESHWAJI WA MIRADI
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb), amemuagiza Mkandarasi wa kampuni ya CHICO anayejenga barabara ya Makutano ya Ntyuka - Mvumi - Makutano ya Kikombo yenye urefu kilometa 76 na Barabara ya Chololo - Mapinduzi (Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi - TPDF) yenye urefu wa kilometa 5, kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unapiga hatua katika utekelezaji wake ifikapo mwishoni mwa mwezi wa pili.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri Bashungwa, amemuagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa anamaliza ujenzi wa sehemu ya barabara ya Kikombo - Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi - TPDF (Km 16), katika kipindi kilichopangwa.
"TANROADS msimamieni huyu CHICO afanye kazi usiku na mchana, sitaki kuona ucheleweshaji wa mradi huu kwa sababu ya fedha, kuna miradi ambayo wakandarasi wake wanadai fedha lakini bado inaendelea", amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amechukizwa na kusuasua kwa miradi hususan inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo kwani fedha za utekelezaji wake zipo na hivyo kusisitiza miradi kuendelea kutekelezwa kwa mujibu wa mikataba na kukamilika kwa wakati na kwa ubora.
Halikadhalika, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Colman Gaston, amesema hadi kufikia tarehe 15 Januari, 2024 utekelezaji wa Mradi huo umefikia asilimia 47 ikilinganishwa na asilimia 81 za mpango kazi wa Mkandarasi ambapo yuko nyuma kwa asilimia 34.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma imeweka utaratibu wa usimamizi na ukaguzi wa mradi huo mara kwa mara pia imeweka wahandisi wawakilishi wa Mwajiri (Counterpart staff) ambao wapo muda wote wa kazi kuhakiksha kazi zinafanyika kwa viwango vinavyotakiwa na ubora elekezi kulingana na mkataba.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, amesema wamejipanga kuhakikisha wanasimamia miradi ya nchi nzima inajengwa kwa kuzingatia ubora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amemuahidi Waziri Bashungwa kuwa watahakikisha wanatunza miundombinu ya barabara na miradi mingine kwani Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo.