Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

WANAFUNZI WAFUNDISHWE NIDHAMU BORA NA TAMADUNI ZA KITANZANIA: BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb) ametoa wito kwa Wazazi, Walezi na Walimu kuwalea, kuwaandaa na kuwafundisha Wanafunzi katika misingi ya nidhamu bora na tamaduni za kitanzania ili iweze kufaa katika jamii na kuwa na mchango kwa Taifa kupitia taaluma zao.

Bashungwa ameeleza hayo tarehe 29 Novemba, 2024 Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza katika Sherehe za Mahafali ya tisa (9) ya Kidato cha Nne ya Shule za Sekondari za Musabe ya Wavulana na Wasichana ambapo jumla ya wanafunzi 410 wamehitimu.

“Kama ilivyosomwa katika Risala naungana na ninyi kwamba nidhamu ndio msingi wa kila kitu, watoto wetu wakilelewa katika misingi bora ni maandalizi mazuri ya kuwafanya waweze kupokea matunda ya taaluma nzuri na hapa nimeona takwimu za miaka yote hapa ni divisheni one na two, Msione vinaelea vimeundwa.”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameupongeza uongozi wa Shule za Musabe kwa jitihada kubwa wanazofanya za kuwaandaa Wanafunzi kitaaluma pamoja na kuweka utaratibu wa kuwafundisha, kuthamini na kutukuza mila na desturi zetu za asili kupitia makabila mbalimbali.

Bashungwa amepokea ombi la uongozi wa Shule hizo kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji na kueleza kuwa tayari amewasiliana na Waziri wa Maji, Juma Aweso na ameahidi kutuma timu ya watalaam kufika na kuangalia namna ya kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Shule zote mbili.

Aidha, Bashungwa ameeleza mipango ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuondoa adha ya foleni ya magari kwa wananchi wa jiji la Mwanza kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo - Busisi) na mpango wa kupanua barabara kuanzia Mwanza Mjini - Nyegezi hadi Roundabout ya Usagara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule za Sekondari za Masabe, Daniel Damian ameeleza kuwa mafanikio ya Shule za Musabe unatokana na kuwa na timu ya walimu na watumishi wanaojituma na wachapakazi na amewahakikishia wazazi na walezi watoto wote 410 waliohitimu Kidato cha Nne kupata ufaulu mzuri kutokana na maandalizi mazuri waliyopewa.

Akisoma Risala ya Shule, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Masabe, Innocent Kiruho ameeleza Shule za Musabe zinajitahidi kwa kiasi kikubwa kudhibiti nidhamu ya wanafunzi kwa kutambua kuwa bila nidhamu hakuna taaluma wala elimu bora na kubainisha Shule hizo zimeendelea kuwa na mafanikio mazuri kitaaluma katika mitihani ya Taifa  kwa miaka mitatu mfululizo.

Ameeleza mipango ya uongozi wa Shule hizo ikiwemo kuendelea kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza ufundishaji wa lugha ya Kichina kwa mwaka wa masomo Januari, 2025 ili wanafunzi wanapohitimu wawe na ujuzi wa lugha tofauti tofauti.