Habari
WADAU WA MIUNDOMBINU WATAKIWA KUISHAURI KIKAMILIFU SERIKALI

Serikali imewataka wadau wa miundombinu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kutumia vyema fursa ya mikutano inayowakutanisha kwa pamoja ili kuweka mikakati endelevu na inayotekelezeka ili kuboresha mikataba ya uendelezaji wa miundombinu ya barabara katika nchi zao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina na warsha ya siku tano iliyozikutanisha nchi zaidi ya 5 za Afrika, Serbia na Marekani inayofanyika Jijini Arusha, Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete ameeleza pamoja na jitihada mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imezichukua ni pamoja na kutilia mkazo mpango mikakati mbalimbali ya utekelezaji kupitia sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo.
“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo mtandao wa barabara nchini Tanzania umefikia zaidi ya kilometa laki moja na elfu themanini (180,000) ukijumuisha barabara za ndani na za wilaya sasa ili kujenga kwa lami barabara zote lazima kama wataalam kupitia uzoefu mtakaupata hapa kutoka maeneo mbalimbali barani Afrika na muutumie uzoefu huo kuishauri Serikali namna bora ya kuendeleza na kuisimamia miundombinu yetu nchini’ amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amesema uwepo wa miundombinu bora nchini utachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi na jamii kwani bidhaa zitatoka kwenye uzalishaji na kuwafikia walaji kwa wakati na hivyo kuinua pato na kuongeza mzunguko wa fedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tanzania Roads Association (TARA) Joseph Odo Haule amesema kwa kutumia mkutano huo unaohusisha wadau kutoka Nchi mbalimbali na utaalam tofauti Chama hicho kitachukua maoni na uzoefu na kuishauri ipasavyo Serikali kwenye maeneo yote ya ujenzi, usimamizi na utafutaji wa fedha za ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Mkutano huo ulioratibiwa na TARA wa wataalam wa miundombinu umezikutanisha nchi za Malawi, Ghana, Zambia, Africa Kusini, Kenya, Namibia, Serbia na Marekani kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika ujenzi, usimamizi na uendelezaji wa mikataba ya miundombinu ya barabara barani Africa.