Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ULEGA ATANGAZA NEEMA KWA WAKANDARASI WAZAWA


* Kupewa miradi yote yenye thamani ya mpaka sh bilioni 50

* Ni maelekezo ya Rais Samia

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuanzia sasa miradi yote ya ujenzi ambayo thamani yake haizidi shilingi bilioni 50 kipaumbele kitakuwa ni wakandarasi wazawa.

Akizungumza katika mkutano na wakandarasi wazawa uliofanyika Dodoma leo, Ulega alisema uamuzi huo unatokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka wakandarasi wazawa wapewe miradi mingi ya ujenzi ili wakue na kukuza uwezo wa kufanya miradi mikubwa zaidi.

Katika kuonyesha dhamira ya dhati ya serikali katika kutimiza azma hiyo, Ulega  amesema Serikali imeingia mikataba ya takriban shilingi bilioni 554.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya dharua iliyoathriwa na mvua za El- Nino na Kimbunga Hidaya ambapo kati ya mikataba hiyo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 412 sawa na asilimia 74 inatekelezwa na wakandarasi wazawa.

“Baada ya Mheshimiwa Rais kutupatia fedha za kurejesha miundombinu yote iliyoharibiwa na mvua, maelekezo ya moja kwa moja ni kuhakikisha miradi yote inafanywa na wazawa na  kuitekeleza miradi hiyo vizuri”,  amesema Ulega.

Katika hatua nyingine, Ulega amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Aisha Amour kuhakikisha  malipo kwa wakandarasi wa ndani yanapewa kipaumbele pale uwezo wa kulipa unapopatikana.

“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha fedha za malipo ya madeni zinalipwa kwa wakandarasi wa ndani kama kipaumbele,”, amesema Ulega

Waziri Ulega ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imeandaa  mikakati ya kuwasaidia Wakandarasi wazawa na Washauri Elekezi  ili waweze kunufaika kupitia miradi inayotolewa nchini na kuwataka watendaji wa Wizara kutoa ushirikiano na kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakwamisha wakandarasi wa ndani kupata miradi.

Kuhusu sulala la malipo, Waziri Ulega amesema kuwa Serikali inaendelea na malipo ya wakandarasi wa ndani kwa kadri inavyopata fedha na amewahakikishia kuwa watalipwa fedha zote wanazodai.

Ulega ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango wa wakandarasi wa ndani kwani wamekuwa msaada mkubwa wakati wa urejeshaji wa mawasiliano ya barabara na madaraja mara baada ya miundombinu hiyo kuathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi, Rhoben Nkori, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwainua wakandarasi wazawa kwani changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwakabili wakandarasi hao zimeshafanyiwa kazi ikiwemo sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024 ambapo imetoa nafasi kwa wazawa kutekeleza miradi mikubwa zaidi  hadi kufikia thamani ya Bilioni 50.

Akitoa neno la shukrani, Mkadiriaji Majenzi Samuel Marwa ameshauri Serikali kupitia CRB ihakikishe kuwa inafanya uhakiki wa kina kutambua kampuni za wazawa ili zabuni za miradi zinazotolewa ziwanufaishe wazawa  husika na si vinginevyo.