Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UJENZI WA MIRADI YA DHARURA LINDI WAENDELEA KWA KASI, MKUU WA TECU ARIDHISHWA


Mkuu wa Kitengo cha Ushauri wa Kihandisi cha Wakala ya Barabara Tanzania (TECU), Mhandisi Lutengano Mwandambo, ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya dharura mkoani Lindi.

Mhandisi Mwandambo amesema hayo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi 13 ya madaraja, boksi kalvati na barabara katika mkoa huo, ambayo kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024 yaliathiriwa na mvua kubwa za El Nino pamoja na kimbunga Hidaya, vilivyosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na kukatika kwa mawasiliano.

Amesema katika barabara kuu ya Lindi–Dar es Salaam pekee kuna miradi mikubwa mitano, ambapo madaraja na kalvati yaliharibiwa vibaya na maji ya mafuriko.

Ameeleza kuwa madaraja hayo sasa yanajengwa upya kwa kunyanyua tuta la barabara pamoja na kujenga makalvati yenye midomo mipana na barabara za maungio ili kuongeza uwezo wa kupitisha maji kwa wingi.

Ameitaja miradi yote inayotekelezwa mkoani Lindi kuwa ni Ujenzi wa Daraja la Somanga Mtama (mita 60), Daraja la Zinga (mita 18), Daraja la Kimambi (mita 39), Daraja la Nangano (mita 25), Daraja la Mbwemkuru II (mita 64), Daraja la Nakiu (mita 70), Daraja la Njenga–Matandu (mita 60), Daraja la Kipwata (mita 40) na maboksi Kalavati mawili, Daraja la Mikereng’ende (mita 40) na maboksi kalvati matatu.

Ameongeza kuwa kazi yinyingine ni ujenzi wa Boksi Kalavati la Mbwemkuru I (mita 20), Daraja la Miguruwe (mita 39) na maboksi kalvati manne, Daraja la Kigombo (mita 25) na boksi Kalavati moja pamoja na maboksi Kalavati sita katika Barabara ya Tingi Kipatimu.

Mhandisi Mwandambo amesema ujenzi wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya dharura inayotekelezwa katika mikoa 22 ya Tanzania Bara, chini ya mpango wa CERC (Contingency Emergency Response Component), ambapo inatekelezwa na makampuni ya wakandarasi wazawa 70 na makampuni 11 kutoka nje ya nchi.