Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UJENZI WA BARABARA YA KIMARA - MAVURUNZA - BONYOKWA - KINYEREZI KWA KIWANGO CHA LAMI WAANZA


Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza ujenzi wa Barabara ya Kimara - Mavurunza - Bonyokwa hadi Kinyerezi (Km 7) kwa kiwango cha lami, jijini Dar es Salaam. 

Ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa na kampuni ya kizawa ya Nyanza Road Works, ambapo barabara hiyo inatarajiwa kurahisisha huduma za  usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa  Ubungo na Segerea jijini humo pindi itakapokamilika.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo ya Kimara, Bonyokwa, Kinyerezi, na maeneo jirani wameeleza kuwa, wana matumaini makubwa kuwa ujenzi huu utapunguza changamoto za miundombinu na usafiri. 

Pia, wanatarajia kunufaika kiuchumi kupitia fursa zitakazotokana na mradi huu, ikiwemo biashara na huduma nyingine zinazotokana na uboreshwaji miundombinu bora ya barabara.

Ujenzi wa mradi huo unajumuisha daraja kubwa lenye urefu wa mita 25, pamoja na madaraja madogo saba ya kalvati, ambayo yatasaidia kupitisha maji wakati wa mvua kubwa. 

Aidha, mradi huo utahusisha ufungaji wa taa za barabarani, hatua inayolenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara hii.

Mradi huu unalenga kuimarisha miundombinu ya jiji, kuboresha huduma za usafiri, na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake.