Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UJENZI BRT II WAFIKIA ASILIMIA 66.6


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT II), Awamu ya Pili kutoka Mbagala hadi Gerezani umefikia asilimia 66.6 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2023.

Prof. Mbarawa amesema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo ambapo amefafanua kuwa kazi zinaenda vizuri huku ikitarajiwa kuwa mradi huo kukamilika kwa muda uliopangwa ili uweze kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri.

“Nimefurahi kazi inaenda vizuri ila bado nitakuwa nikija hapa kukagua mradi huu mara kwa mara ili kuhakikisha mkandarasi anamaliza kwa wakati na viwango kwa sababu mradi huu ni muhimu sana katika kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha upande wa pili wa barabara za juu (flyover) ya Chang’ombe na Kurasini ifikapo mwezi Oktoba ili kuruhusu magari kupita juu huku kazi nyingine zilizobakia zikiendelea.

Amemtaka pia kukamilisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 80 eneo la BP ifikapo mwezi Desemba 2022 na madaraja mengine kukamilishwa mwezi Januari, 2023 ili kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika maeneo hayo.

Pamoja na hayo amewataka wananchi waliopo karibu na mradi huo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili mradi huo umalizike mapema iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT II), Eng. Frank Mbilinyi, amesema kuwa wanatarajia Daraja lililopo Bandarini kumalizika na magari kuanza kupita mwezi Oktoba mwishoni wakati madaraja mengine yameshakamilika kwa upande mmoja na magari yameruhusiwa kupita.

Mradi huu ni moja ya mkakati ya Serikali ya kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam ambapo unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 20.3, Daraja kubwa la Waenda kwa miguu eneo la Mbagala, vituo vya mabasi 27, karakana ya mabasi 1, vituo vikuu viwili vya mabasi (Terminals) eneo la Kariakoo na Mbagala, vituo vya mlisho (feeder station) 5 pamoja na barabara za juu (flyover) 2 eneo la Chang’ombe na Uhasibu ambazo zitagharimu takribani Shilingi Bilioni 217.