Habari
TPA NA TRC YAANZA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA MAKAMU WA RAIS BANDARI YA TANGA

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA) na Shirika la Reli Nchini (TRC) imeanza mara moja ukarabati na urejeshwaji wa reli inayoanzia stesheni ya reli Tanga kuelekea Bandarini jijini humo ili kuhakikisha mzigo unashushwa bandari hapo na kuwafikia walaji kwa wakati.
Kazi hiyo imefanywa siku moja baada ya maelekezo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Mpango kuelekeza TPA na TRC kukarabati na kurejesha reli inayotoka stesheni ya treni Tanga kuelekea Bandarini wakati alipotembelea mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya kazi hiyo Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Serikali itaendeleea kutekeleza maelekezo na mipango yake katika miradi mbalimbali ili kuhakikisha malengo iliyojiwekea yanatimia kwa wakati.
“Niwapongeze sana TRC na TPA kwa uharaka wa kutekeleza maelekezo ya viongozi, na hii iwe kianzio kwa wataalaam kufanya kazi zao kwa wakati maana nimeona hapa tayari mmeanza kazi na muhakikishe inakamilika ndani ya muda mfupi na treni inaanza kutoa huduma bandarini’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amewataka TRC na TPA kushirikiana kwenye utendaji kwani ufanisi wa utendaji unategemea baina ya taasisi hizo na kuwasisitiza kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kumaliza changamoto mbalimbali za huduma zilizopo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uendeshaji kutoka TRC, Focus Sahani, amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya wiki mbili na treni kuanza majaribio ili kupima mapungufu yaliyopo na kuyarekebisha kabla ya kuhudumia mizigo bandarini.
Kaimu Mkurugenzi Sahani ameongeza Shirika linaendelea na ukarabati wa mabehewa ili kuhakikisha mzigo unaopitia bandarini unahudumiwa kwa wakati na kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo baina ya Mkoa huo na mikoa ya karibu.