Habari
TBA YAPONGEZWA KULETA TIJA MAHALI PA KAZI

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umepongezwa kwa jinsi unavyoshirikisha wafanyakazi wake kutambua shughuli zake kupitia Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi.
Akifungua Mkutano wa Baraza la wafanyakazi TBA, unaofanyika jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya ujenzi Mhandisi Balozi Aisha Amour, amebainisha kuwa, suala la kushirikisha wafanyakazi kutambua shughuli zinazotekelezwa na Wakala ni jambo muhimu ambalo linasaidia kuleta tija katika utendaji kazi.
Aidha Mhandisi Aisha, amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi kuzingatia maadili katika utumishi wa umma na vita dhidi ya rushwa.
Awali akiongea katika Mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameeleza kuwa Mkutano huo pamoja na mambo mengine pia utatoa elimu kuhusu masuala ya rushwa na utawala bora, afya ya akili na namna ya kuepuka msongo mawazo, elimu kuhusu magonjwa na athari zitokanazo na magonjwa yasiyoambukizwa.
Mkutano wa Baraza la wafanyakazi unahusisha wajumbe kutoka Menejimenti ya TBA na wajumbe kutoka Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) Tawi la TBA. Mkutano huu wa Baraza la Wafanyakazi utafanyika kwa siku mbili kunzia Mei 11 mpaka 12, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.