Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TBA ENDELEENI KUSIMAMIA MIRADI KWA UBORA - DKT. MSONDE


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt.Charles Msonde, ametoa wito kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuendelea kusimamia miradi ya ujenzi wa majengo ya Serikali kwa viwango vya juu na kuhakikisha inakamilika kwa ubora unaotakiwa.

Dkt. Msonde ametoa maelekezo hayo alipokutana na wafanyakazi wa TBA mkoani Dodoma, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uzalendo.

"TBA mnafanya kazi nzuri inayoonekana moja kwa moja kwa wananchi. Mnasimamia vyema majengo ya Serikali, ndiyo maana yako imara na hayaanguki. Hivyo, endelezeni juhudi hizo kwa bidii na uadilifu," amesema Dkt. Msonde.

Aidha, amewataka wafanyakazi wa TBA kuendelea kujifunza ili kuongeza maarifa yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Meneja wa TBA mkoa wa Dodoma, Qs.Emmanuel Wambura, amesema wakala huo unaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 3,500 za makazi mkoani Dodoma.

"Kwa sasa tumejenga nyumba 150 katika awamu ya kwanza na tunaendelea na awamu ya pili ambapo nyumba 150 nyingine zinajengwa, kati ya hizo, nyumba 100 zitakuwa za ghorofa," ameeleza Wambura.

Mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi huku ukitekelezwa kwa awamu kulingana na mpango wa Serikali wa kuimarisha sekta ya makazi nchini.