Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TASAC YAKABIDHI MABOYA KWA WANAFUNZI


Shirika la Uwakala  wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa maboya zaidi ya 25 kwa wanafunzi wa shule za msingi za Rumuri Kashai, Nyamkazi wanaolazimika kutumia usafiri wa maji kila siku kwenda shuleni katika visiwa vya Msira ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wanakuwa salama.

 

Akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya siku ya mahabaria mkoani Kagera Katibu Tawala wa Mkoa huo, Profesa  Faustine Kamuzora, ameipongeza TASAC na kusema kuwa pamoja na juhudi hizo Serikali imeendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa meli ili kuhakikisha wakazi wa Kanda ya Ziwa wanakuwa na usafiri wa uhakika kwa njia ya maji.

 

“Niwapongeze kwa juhudi mnazozifanya za kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu sahihi na watoto wetu kupata vifaa vitakavyowasaidia wanapotumia usafiri wa  majini ila niwaombe pia tuendelee kutoa elimu zaidi ili kuendelea kuepusha vifo vinavyowezajitokeza kutokana na ukosefu wa vifaa sahihi vya majini", amesema Prof. Kamuzora.

 

Prof. Kamuzora amewataka wananchi na wanafunzi hao kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu kwani vimenunuliwa kwa kutumia fedha za Serikali.

 

Kwa upande Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Kapteni Musa Mandia, amesema Wakala pamoja na kazi za udhibiti unaendelea kusimamia viwango vya mabaria ili kuhakikisha wanapata vyeti vyenye sifa za kuwaruhusu kuajiriwa ndani na nje ya nchi.

 

Kapteni Mandia ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza fedha kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), ili kuhakikisha Sekta inapata watalaam wa kutosha mkakati unaoenda sanjari na ujenzi wa meli katika maziwa nchini.

 

Naye, Meneja wa Masoko na Elimu kwa Umma, Bi. Josephine Bujiku, ambaye alimuwakilisha MKurugenzi Mkuu wa TASAC amesema kupitia maonesho hayo TASAC imewafikia zaidi ya wananchi 3000 kwa kuwapa elimu ya usalama ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.

 

Siku ya mabaharia huadhimishwa Kimataifa kila ifikapo 21-25 Juni kila mwaka ambapo kwa mwaka huu yamefanyika Kitaifa Mkoani Kagera na yamebeba  kauli mbiu ya “Safari yako leo na kesho, toa ushirikiano".