Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS YATEKELEZA KILOMETA 238.9 ZA BARABARA ZA LAMI


Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora imesema imejenga barabara zenye urefu wa kilometa 238.9 kwa kiwango cha lami ambazo zimegharimu zaidi ya  bilioni 300 na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari  Kaimu Meneja wa TANROADS  mkoa wa Tabora, Mhandisi Rwegoshora Michael walipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Kazilambwa - Chagu (km 36) kwa kiwango cha lami ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 89.62 kwa gharama ya shilingi Bil 36.9 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023.

Mhandisi Rwegoshora amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utaiunganisha mkoa wa Tabora na Kigoma kwa upande wa Tabora ambapo ndio kipande kilichobakia kuunganishwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, ameeleza mradi huo unatekekelezwa na mikoa miwili ambapo kwa upande wa Tabora wanajenga kilometa 26 na kwa upande wa Kigoma wanatekeleza kilometa 10.

Ametaja miradi iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami mkoani humo ikiwemo  barabara ya Tabora - Koga - Mpanda sehemu ya Usesula - Komanga yenye urefu wa kilometa 117.5 na barabara ya Nyahua - Chaya yenye urefu wa kilometa 85.4.

“Tunaishukuru Serikali  kwa kutekeleza kwa vitendo sera yake ya kuunganisha mikoa na wilaya kwa barabara kwa kiwango cha lami maboresho hayo yana matokeo ya moja kwa moja kwani bidhaa nyingi zitawafikia walaji kwa wakati lakini huduma zitaboreka hususani usafirishaji", amesema Kaimu Meneja.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma Mhandisi Ngoko Mirumbe amesema mradi huo ukikamilika utapunguza muda wa usafiri wa kilometa 300 kutokea Dar es Salaam.

"Zamani watu wa Kigoma walikuwa wanasafiri kwenda Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Nyakanazi, kukamilika kwa mradi Dar es Salaam hadi Kigoma (kwa baadhi ya vipande vilivyobaki), zaidi ya kilometa 300 zitakuwa zimepungua, na hii litaleta unafuu kwa usafiri na gharama zitapungua", amefafanua Mhandisi Mirumbe.

 

Amesema barabara hiyo inajengwa na kampuni ya STECOL Corporation na kusimamiwa na Kitengo cha Usimamizi wa Miradi cha TANROADS - TECU.

Amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutawezesha shughuli mbalimbali za usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya nchi ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda na hivyo kuchangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ameongeza kuwa faida hiyo muhimu kiuchumi inatokana na kwamba ujenzi wa barabara hiyo utaiunganisha Mkoa wa Kigoma na Tabora huku ikitatua changamoto ya muda mrefu ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine nchini na hivyo kuwezesha kufika kwa urahisi katika nchi hizo.