Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI BASHUNGWA LA KUPANDA MITI MAENEO YA BARABARANI


Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma imeanza kutekeleza agizo lililotolewa jana Januari 29, 2024 na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa la kupanda miti maeneo ya barabara kwa ajili ya kuendelea kupendezesha miji nchini na kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Meneja Ofisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani amesema kuwa Ofisi yake inaendelea kutekeleza maelekezo ya viongozi ya kupendezesha mji wa Dodoma na pia imeweka utaratibu wa kuendelea na zoezi hilo katika barabara zake zote.

Mhandisi Zuhura amesema leo Januari 30, 2024 Jijini Dodoma, mara baada ya kumaliza zoezi la upandaji miti na kusisitiza kuwa jumla ya miti waliyoipanda toka mwaka 2022 ni takribani 2,089 na mwaka huu wa fedha wamepanga kuendelea na zoezi hilo ambapo watapanda miti 540 ndani ya jiji hilo.

"Leo hii tunatarajia kupanda miti 114 ambayo tumeiandaa na wafanyakazi wote wa TANROADS wamejipanga na tupo tayari kufanya zoezi hili", amefafanua Mhandisi Zuhura.

Amesema miti hiyo waliyoipanda wataendelea kuitunza kwa kuhakikisha kwamba inakua na inafikia malengo ambayo wamejiwekea na kusisitiza kuwa ingawa kuna changamoto ya hali ya hewa lakini watahakikisha wanaendelea kuitunza miti kwa kuimwagilia maji wakati wa kipindi cha kiangazi.

"Mkoa wetu wa Dodoma una kipindi kirefu sana cha kiangazi lakini TANROADS tutahakikisha tunaendelea kuitunza na kuiwekea mbolea ili iweze kustawi zaidi" alisema.

Kwa upande wake Mfanyakazi wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Elisony Mweladzi, amesema amehamasika na zoezi hilo la upandaji miti hivyo yeye pamoja na wafanyakazi wengine wataendelea kutekeleza maelekezo yote watakayopewa na viongozi wao kwa kupanda miti mbalimbali inayostahi,ili hali ya hewa ya Dodoma.

Aidha, ametoa wito kwa Wananchi kupanda miti na kuitunza ili iweze kupendezesha mandhari ya mji wa Dodoma na kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

"Tunatoa wito kwa kila kaya iweze kupanda miti angalau sita (6) pamoja na kuitunza kwa kuimwagilia maji, kuiwekea mbolea na kuzuia mifugo mbalimbali kutoiharibu miti hiyo",

Mweladzi pia amewasihi wananchi wote wa Dodoma kutokutupa takataka kwenye vyanzo vya mito, makalavati na pia barabarani kwani vitendo hivyo hupelekea uharibufu wa Mazingira.