Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS YAKAMILISHA MATENGENEZO YA BARABARA YA MOROGORO-IRINGA


Serikali kupitia TANROADS imekamilisha kufanya ukarabati na maboresho ya barabara ya Morogoro kuelekea Iringa (Tanzam Highway) kwa kutenga fedha kwa mpango wa haraka ili kunusuru barabara hiyo kukatika katika eneo hatarishi la Iyovi ambalo kingo za mto Ruaha zimekutana na tuta la barabara na lina miteremko na kona kali.

Hayo yamebainika leo tarehe 18 Julai 2023, baada ya Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro Mhandisi Mussa Kaswahili kutembelea eneo hilo na kuzungumza na vyombo vya Habari kwa niaba ya Meneja wa TANROADS Mkoani humo Mhandisi Alinanuswe L. Kyamba.

Mhandisi Kaswahili amesema katika msimu wa mvua zilizoisha mwezi April mwaka huu 2023, zilisababisha madhara katika eneo hilo baada ya maji ya Mto Ruaha kujaa na kugonga tuta la barabara  na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa na kupelekea barabara kutishia kukatika hali ambayo isingedhibitiwa mapema ingeweza kukwamisha Shughuli za usafiri na usafirishaji katika barabara hiyo ambayo inaunganisha Tanzania na Nchi jirani za Zambia na Congo.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo Serikali chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Mtendaji Mkuu wa TANROADS ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Barabara ilitenga fedha za haraka kiasi cha shilingi milioni 480 kwa ajili ya ukarabati na maboresho ya kingo za barabara hiyo na baada ya taratibu zote ikampa kazi Mkandarasi mzawa wa kampuni ya CGI Construction Company Limited ambaye amekamilisha kazi kwa wakati na muda uliopangwa.

Amesisitiza kuwa barabara hiyo ni moja ya barabara zinazotumiwa na wasafirishaji wanaopokea mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, hivyo ni Jicho la Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kwa ujumla inaangaliwa kwa ukaribu na inahudumiwa kama kipaumbele cha kwanza katika kila bajeti inayotengwa kila mwaka kwa Mkoa wa Morogoro na inapohitajika fedha za dharura hutengwa ili kuhakikisha barabara hiyo na nyingine zenye umuhimu kama hiyo zinakuwa salama na zinapika wakati wote pasipokuwa na changamoto yoyote.

Mhandisi Kaswahili ameongeza kuwa "TANROADS tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kutenga fedha na kuzipeleka maeneo mbalimbali ikiwemo mkoa wa Morogoro kwa ajili ya maendeleo na matengezo ya barabara, Rais hajahi kuacha kutuletea fedha, Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa Serikali ipo makini inawajali ipo pamoja na wao na ipo kwa ajili ya kutekeleza miradi kuhakikisha hawapati changamoto yoyote kwenye eneo la miundombinu hasa ya barabara".