Habari
TANROADS WAASWA KUWA WABUNIFU KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wameaswa kuwa wabunifu na mstari wa mbele katika ulindaji wa miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali pamoja na kutumia malighafi zinazopatina sehemu husika ili kupunguza gharama zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na mizani hapa nchini.
Agizo hilo limetolewa mkoani Njombe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Mhandisi Aisha Amour, katika kikao kazi na watumishi wa Wakala huo ambapo amesisitiza weledi, ubunifu, matumizi ya kisasa ya TEHAMA ili kuleta ufanisi katika utendaji wao kazi.
“Nahitaji mabadiliko kwa watumishi wa TANROADS katika matumizi ya teknolojia maana huko kuna vitu vingi vya kujifunza badala ya kupoteza muda kuangalia masuala yasiyokuwa na tija katika utendaji kazi wenu”, amesisitiza Balozi Aisha.
Ameongeza kuwa Wizara imepanga kutoa motisha kwa watumishi ambao watakuja na mawazo mapya yenye kuleta tija katika uboreshaji na usimamizi wa miundombinu iliyopo na inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
“Hakikisheni mnaibua vipaji vya watumishi wenu mahala pa kazi kwa kuhakikisha kila mtumishi aliyeajiriwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo na kuondoa dhana ya watu wachache kuonekana bora zaidi”, amesema Katibu Mkuu huyo.
Awali akitoa taarifa ya mkoa huo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Kipembawe Msekwa ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Njombe – Makete na Itoni – Ludewa – Manda zinazounganisha Makao Makuu ya Mkoa na Wilaya (Ludewa na Makete) tayari zimeanza kutoa matunda katika shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao kutoka shambani na kukuza uchumi wa mkoa.
“Barabara hizi zimepelekea muda wa safari kupungua hadi wastani wa saa mbili (kutoka Makete) na saa tatu (kutoka Ludewa) ambapo hapo awali hasa kipindi cha masika muda wa safari ulikuwa ni mwendo wa siku nzima”, amefafanua Mhandisi Msekwa.
Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Njombe unahudumia matengenezo ya barabara yenye jumla ya (km 1,188.23) kati ya hizo (km 403.420) ni Barabara Kuu na (km 784.810) ni Barabara za Mkoa