Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAWAHIKIKISHIA MAZINGIRA MAZURI WAMILIKI WA MALORI TANZANIA


Serikali imewaahidi wamiliki wa malori nchini kuwa itaendelea kutafuta ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuhakikisha usafiri na usafirishaji unafanyika katika mazingira rafiki na wezeshi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA) jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete, amesema jitihada zilizofanyika ili kurahisisha usafirishaji ni pamoja na kupunguza mizani ya upimaji kutoka 7 hadi 3 kwa mizigo inayokwenda nje ya nchi.

“Serikali inajali sana wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi na tunatambua kuwa kuna nchi zaidi ya 4 zinazotumia bandari ya Dar es Salaam hivyo nyinyi kama wamiliki tunawahakikisha kuwa tutatumia kila jitihada kuwe na mazigira rafiki ili msikwamishe mizigo kufika kwa wakati’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema Serikali iko kwenye hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa barabara ya Igawa hadi Tunduma inaongezwa upana ili kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika barabara hiyo.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wamiliki wa Malori Zambia (ZAFFA),Trodson Chemu, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao Tanzania imeendelea kuuonyesha hususani katika kutatua changamoto za wasafirishaji wa malori hasa kwa upande wa mpaka wa Zambia.

Rais Chemu ameongeza kuwa ushirikiano ambao umeonyesha baina ya nchi hizo umekuwa na manufaa sana kwa wasafirishaji kwani tayari changamoto zimeanza kupata ufumbuzi ikiwemo kupunguza muda kwa malori hayo kukaa mpakani Tunduma.

Naye Mwenyekiti wa TAMSTOA Chuki Shambani, ameiomba Serikali  kupitia mapendekezo yaliyowasilishwa na chama hicho kwa Serikali kuhusu punguzo la kodi zinazotozwa kwa malori mapya yanayoshushwa kupitia bandari ya Dar es Salaam lengo likiwa kutoa nafasi kwa wamiliki wengi zaidi kumiliki magari ya mizigo.

Chama cha TAMSTOA ni miongoni mwa vyama vya wasafirishaji ambacho kimeanzishwa mwaka 2014 kwa kuwa na wanachama 40 na kwa sasa kimefikia wanachama takribani 700.