Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAPATA SULUHISHO LA MLIMA KITONGA: BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema Serikali imesikia kilio cha Watumiaji wa barabara kuu ya TANZAM kutokea Ruaha Mbuyuni hususan eneo la Mlima Kitonga lenye urefu wa kilometa 7.6 na inakwenda kutoa suluhisho, ambapo tayari wataalam wamewasilisha mapendekezo ya muda mfupi na muda mrefu ambayo yatafanyiwa kazi na Serikali.

Eneo hilo la Mlima Kitonga ambalo limekuwa kero kubwa kwa watumiaji wa barabara kutokana na kuwepo kwa mlima mkali na kusababisha foleni kwa  muda mrefu pamoja na ajali za magari sasa Serikali inakwenda kuipanua kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.478 ikiwa ni makadirio ya utekelezaji wake katika mpango wa muda mfupi.

Bashungwa amesema hayo mkoani Iringa wakati alipofika eneo hilo na kupata taarifa ya wataalam kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) mara baada ya kukamilisha usanifu wa upanuzi wa Mlima Kitonga ili kuimarisha usalama kwa watumiaji wa barabara hiyo.

"Moja ya maagizo aliyonipatia Mheshimiwa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kushughulikia kero ya eneo hili la Mlima Kitonga ambalo limekuwa likipoteza ndugu zetu pamoja na mali na ameniagiza kwanza tutafute suluhisho la muda mfupi na nimpelekee suluhisho la muda mrefu", amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa wananchi wa mkoa wa Iringa, Mikoa ya jirani pamoja na nchi zinazotumia barabara hiyo wakae tayari kwani Mheshimiwa Rais ni mtu wa vitendo na tayari utekelezaji wa upanuzi utaaanza hivi karibuni.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Iringa, Mha. Yudas Msangi ameeleza kuwa jumla ya mita 1600 za Mlima Kitonga zitatanuliwa ili kupunguza ajali na foleni katika eneo la Mlima Kitonga Barabara kuu ya TANZAM hiyo ikiwa ni suluhisho la muda mfupi.

Ameongeza kuwa maeneo mengine yatafungwa  vioo maalum kwenye maeneo yenye kona kali ili kuweza kuwasaidia  madereva kuona magari mengine na kuongeza usalama zaidi.

Kuhusu suluhisho la kudumu, Eng. Msangi amesema kuwa tayari wameshasaini mkataba kwa ajili ya usanifu ambapo kulikuwa na mapendekezo ya  kuwa na njia ya mchepuo wa Mlima Kitonga, pamoja na pendekezo la barabara ya Mchepuo Mlowa – Mifugo – Mlafu hadi Ilula yenye urefu wa km 31.

Pendekezo linguine ni kuchoronga mlima wa Kitonga na kupanda handaki la barabara (Tunnel) na kufanya upanuzi wa mlima ili kupata njia nyingi zaidi (Lanes).