Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YAJA NA BARABARA ZA MZUNGUKO WA NDANI DODOMA


Serikali imesema imejipanga kuanza ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani wa Jiji la Dodoma utakaokuwa na urefu wa kilometa 16 kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo linaloendelea kukua kwa kasi kutokana na shughuli za Serikali kuhamia huko.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya wakati akikagua ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 112.3 ambao ujenzi wake unaendelea vizuri.

"Lengo la Serikali ni kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika miji ili maisha ya watanzania yaweze kuimarika na kuendelea kuendesha shughuli zao za kimaendeleo kwa wakati", amesema Eng. Kasekenya.

Aidha, amewaagiza Wahandisi Washauri wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje kuhakikisha wanaongeza vifaa vya ujenzi pamoja na wataalam wenye sifa ili kuongeza kasi ya mradi na kuikamilisha kama ilivyopangwa.

Ameagiza pia kwa wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kama ilivyosanifiwa huku akiwasisitiza kufuata viwango vilivyoainishwa katika mikataba.

Kasekenya amewataka TANROADS pia kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi hao kutekeleza kazi za jamii kama ilivyoainishwa katika mikataba ikiwemo ujenzi wa visima vya maji vinne, shule ya msingi  moja, vituo vya afya vinne  pamoja na ununuzi wa gari nne za wagonjwa ili wananchi waendelee kunufaika navyo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma Eng. Salehe  Juma ameeleza kuwa sehemu ya mradi  ya Nala - Veyula - Mtumba (km 52.3), imefikia asilimia 22.54 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba, 2024 na upande wa sehemu ya Bandari Kavu ya Ihumwa - Matumbulu - Nala (km 60), imefikia asilimia 16.48 na kutarajiwa kukamilika ifikapo Machi, 2025.

Eng. Juma ameeleza kuwa mpaka sasa wakandarasi na wahandisi washauri hawadai chochote kwani malipo yanaenda vizuri na wote wapo katika hatua mbalimbali ya ujenzi wa matuta ya barabara pamoja na ujenzi wa madaraja.

Kwa upande wa ajira amesema kuwa mradi umetoa fursa ya ajira kwa watu 902 kwa mradi mzima ambapo watanzania 723 wamepata fursa hiyo.

Mradi wa ujenzi wa barabaraa ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi Bilioni 220.