Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI YADHAMIRIA KUFUNGUA BARABARA YA LUTEBA HADI IPELELE


Serikali imeamua kufungua barabara ya Luteba hadi Ipelele yenye urefu wa kilomita 9 kwa kiwango cha changarawe kwa ajili ya kuunganisha Wilaya za Makete na Rungwe na hivyo kurahisisha shughuli  za usafirishaji wa abiria,  mazao ya kilimo na utalii kupitia hifadhi ya Kitulo.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo ambayo haikuwepo kabla Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ameupongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kwa kuhakikisha barabara hiyo inaanza kujengwa na hatimaye kuruhusu hata wananchi kuipita.

“Niwapongeze Mameneja wa Njombe na Mbeya kwa kushirikiana katika kazi hii kwani maeneo haya hayakuwa kabisa na barabara na wananchi walilazimika kutembea kwa mguu kufuata mahitaji muhimu kutoka katika vijiji ambavyo viko Jirani kwa Wilaya hizi mbili", amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amewataka wadau mbalimbali kuanza kuwekeza katika Hifadhi ya Kitulo kwani miundombinu imeanza kuboreshwa ambapo itakapokamilika itachangia kwa kiasi kikubwa pato la mkoa na kukuza utalii.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Beda, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika maboresho ya miundombinu na kusema kukamilika kwa barabara kutaongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika Wilaya hizo mbili na hivyo kuinua pato la wananchi, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Matari Masige, amesema mpaka sasa ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 80 na kazi zote zinatarajiwa kukamilishwa mwisho wa mwezi Julai.

Mradi wa kufungua Barabara wa Luteba hadi Ipelele kwa kiwango cha changarawe unatekelezwa kwa fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 900 na inajengwa na Mkandarasi mzawa  Kampuni ya Narmo Company Limited.