Habari
SERIKALI KUTEKELEZA KWA AWAMU UJENZI BARABARA YA BUKOMBE - KATORO

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema inatekeleza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Bukombe – Katoro (km 58.20) kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo Awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Bukombe (Ushirombo) hadi Bwenda (km 5.3) ambapo zabuni za kumpata Mkandarasi zimefunguliwa tarehe 20 Januari, 2025 na kazi ya tathmini ya zabuni hizo inaendelea.
Aidha, sehemu ya pili kutoka Kashelo hadi Nyikonga (km 10.4) pamoja na Daraja la Nyikonga iko katika hatua ya majadiliano huku Mkataba wa kazi unatarajiwa kusainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Februari, 2025. Kwa sehemu zilizobaki za Bwenda - Kashelo (km 16.3) na Nyikonga – Katoro (km 26.2), Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi.
Hayo yameelezwa Januari 29,2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Rose Busiga aliyeuliza ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Bukombe hadi Katoro kwa kiwango cha lami. “Kabla ya kuijenga Barabara hiyo kwa kiwango cha lami lazıma ijengwe kwa kiwango cha changarawe halafu ifanyiwe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kadri fedha inavyopatikana”, amesema Eng. Kasekenya.
Kadhalika, Serikali inatekeleza Ujenzi wa Barabara ya Katumba – Mbambo – Tukuyu (km 83) kwa awamu. Sehemu ya kutoka Lupaso hadi Mbambo (km 20) ambapo kutoka Kabanja hadi Tukuyu (km 7) ujenzi kwa kiwango cha lami umekamilika.
Sehemu iliyobaki ya kutoka Katumba – Lupaso (km 35.3) na Mbaka – Kibanja (km 20.7) mikataba ya ujenzi imesainiwa na kwa sasa mkandarasi yupo kwenye maandalizi ya kuanza kazi baada ya kulipwa malipo ya awali na kusisitiza kuwa kazi zimepangwa kukamilika mwezi Mei, 2027 kwa sehemu zote mbili.
Eng. Kasekenya amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Rungwe Albert Mwantona aliyeuliza lini Serikali itamaliza ujenzi wa Barabara ya Katumba – Mbambo – Tukuyu.
Kuhusu Ujenzi wa Barabara ya Old Korogwe - Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Maramba hadi Mabokweni amesema kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa Kina wa barabara (km 127.69) iko katika hatua za mwisho ambapo kwa sasa Mhandisi Mshauri anafanya kazi ya kugawa Barabara katika sehemu nne kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji.
“Kazi hii inatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi, 2025. Baada ya kukamilika kwa Usanifu Serikali itaanza ujenzi kwa kadri ya fedha zinavyopatikana”, amesema Kasekenya.
Eng. Kasekenya ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Mjini Dkt. Alfred Kimea aliyeuliza ni lini ujenzi wa Kiwango cha lami Barabara ya Old Korogwe - Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Maramba hadi Mabokweni utaanza.