Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUONGEZA BAJETI YA MATENGENEZO YA BARABARA YA TANDAHIMBA – MTAMA.


Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itaongeza bajeti ya matengenezo barabara ya Tandahimba – Mitevu – Mkunja- Mpwiti hadi Mtama kwa kiwango cha Changarawe na kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya mipango ya baadaye ya kuijenga kwa kiwango cha lami. 

Waziri Bashungwa amesema hayo Septemba 16, 2023 wakati akitoa salamu za Wizara yake mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Majaliwa Tandahimba, wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara. 

“Mhe. Rais kwa niaba yako naomba niwaahidi wananchi wa Mtwara kwamba sisi Viongozi wa Wizara,  tunaenda kuiwekea bajeti barabara hii ili upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uweze kufanyika kwenye bajeti ya mwaka 2024/25  na kuwa katika kipaumbele kwa miaka ijayo kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami”, amesema Bashungwa. 

Waziri Bashungwa amesema katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Wizara itaendelea kushirikiana na wabunge katika utekelezaji wa miradi ya kisekta kwa wakati.