Habari
SERIKALI KUJENGA KWA LAMI BARABARA UNGANISHI MBEYA NA SONGWE
SERIKALI imesema barabara zote za kimkakati zinazounganisha mikoa ya Mbeya na Songwe zitajengwa kwa kiwango cha lami ili kuufungua ukanda wote wa kusini magharibi mwa Tanzania kwa lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema katika kuhakikisha hilo tayari Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 800 ili kuwalipa fidia wananchi watakaoguswa na ujenzi wa barabara ya Isongole-Ndembo hadi Isoko km 52.14 inayounganisha wilaya za Ileje na Kyela.
“Maeneo haya licha ya uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula, miti na uvuvi pia ni maeneo ya mipakani yanayohitaji barabara za uhakika zinazoweza kupitika kipindi chote cha mwaka “, amesisitiza Eng. Kasekenya.
Amezungumzia umuhimu wa wananchi waliolipwa fidia kupisha maeneo ya barabara ili mkandarasi kuanza kazi mapema iwezekanavyo.
“Kama umelipwa fidia ni vizuri ukatafuta eneo jingine ili kuiwezesha Serikali kumkabidhi mkandarasi eneo la mradi na kazi ya ujenzi ianze mara moja,” amesema Naibu Waziri huyo wa ujenzi.
Kuunganika kwa barabara za mkoa wa Songwe na Mbeya kutarahisisha shughuli za uchukuzi na usafiri mipakani na hivyo kuchochea ufanisi katika mipaka na kuwavutia wasafirishaji wengi kutumia bandari za Tanzania.
Amesema kukamilika kwa kiwango cha lami kwa barabara za Mlowo-Kamsamba, Mbalizi-Mkwajuni-Makongolosi, Isongole-Ndembo –Isoko, Ibungu –Kalembo-Katengele-Kafwafwa-Kiwira-Kimo na Igawa-Mbeya-Tunduma kutachochea ukuaji mkubwa wa uchumi wa mikoa ya nyanda za juu kusini na magharibi mwa nchi.