Habari
WATUMISHI WIZARA YA UJENZI WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA BIDII

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Wizara ya Ujenzi Bw. Mrisho Mrisho amehimiza watumishi wa Wizara ya Ujenzi kufanya kazi kwa bidii, umoja na mshikamano ili kuleta tija na matokeo chanya katika kuhakikisha dira na dhima ya Wizara ya Ujenzi inafikiwa kwa ubora, wakati na usalama maeneo ya kazi.
Mrisho ameeleza hayo Mkoani Arusha wakati akifunga mafunzo ya Huduma kwa Mteja katika mazingira ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Wizara ya Ujenzi yaliyotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania campas ya Singida yenye lengo la kuongeza tija na ari katika Utumishi wa Umma.
“Niwatake watumishi wa Wizara ya Ujenzi kufuatia mafunzo hayo mbadilike katika utendaji kutoka katika utendaji wa chini hadi wa kati na wa juu ili ile tija ya kuwahudumia watanzania iweze kupatikana“, amesema Mrisho.
Amewataka Watumishi wa Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi yote waliyofundishwa, waliyokumbushwa na kusisitizwa kuhusu miiko na taratibu mbalimbali za Utumishi wa Umma.
Naye, Mratibu wa Mafunzo hayo, Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi Bw. Onesmo Mkandawile ameeleza kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa mpango wa mafunzo wa Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 na unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu hii ya tatu ya mafunzo imehudhuriwa na jumla ya Watumishi takribani 54.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Mafunzo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Bw. Emmanuel Masewa ameshukuru kwa niaba ya Uongozi wa Chuo kwa Wizara ya Ujenzi kuwaamini na kuwapa fursa ya kutoa mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na Watumishi wa Wizara ya Ujenzi na kuamini kuwa mafunzo hayo yataenda kuongeza chachu na tija katika utendaji wa majukumu yao.