Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUJA NA ‘MASTER PLAN’ YA MIUNDOMBINU.


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inaandaa Mpango Mkuu (Master Plan) wa Miundombinu ya nchi kulingana na mahitaji ya kiuchumi na kijamii itakayowezesha kurahisisha usafiri na usafrishaji kulingana na ongezeko la watu nchini.

Mpango huo utaangazia mtandao wa barabara wa nchi nzima kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Ameeleza hayo Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, leo Januari 8, 2024 wakati alipokutana na Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafiri na Utalii kutoka nchi ya Japan, Mhe. Konosuke Kokuba ambaye ameongozana na watalaamu mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi nchini Japani.

“Miundombinu ya barabara inaenda sambamba na miundombinu mingine kama vile reli, kwa hivyo tutashirikiana na Wizara ya Uchukuzi kuandaa master plan ya miundombinu katika kuhudumia watanzania”, amesema Waziri Bashungwa.

Ameielekeza TANROADS kuandaa majadiliano ya Washauri elekezi na Wakandarasi kutoka Tanzania na nchi ya Japani ambao utakuwa endelevu ili kuendeleza mashirikiano ya karibu katika Sekta hiyo.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo mahsusi ya kuweka mazingira wezeshi kwa Wakandarasi Wazawa ambapo Wizara imeanza kupitia mpango wa manunuzi ambao awali ulikuwa unawabana Makandarasi hao.

Katika mkutano huo, Waziri Bashungwa ameipongeza Serikali ya Japani kwa ushirikiano ambao wameendelea kuutoa tokea nchi ya Tanzania kupata Uhuru na ameendelea kuzialika Sekta Binafsi kutoka nchi hiyo kuendelea kufanya kazi na mkampuni ya Tanzania kwa karibu zaidi ili kubadilishana uzoefu.

Bashungwa amesema ujio wa Waziri huyo umekuja muda sahihi kwani Serikali inakwenda kuiboresha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kama mdau mkubwa wa matengenezo ya magari aina ya TOYOTA ambayo kwa asilimia kubwa yanatumika Serikalini na kuhitaji msaada wa kiufundi (Technical Assisatant).

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafiri na Utalii kutoka Serikali ya Japan, Mhe. Konosuke Kokuba, amesema kuwa Serikali hiyo itaendelea kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo kwa kuendelea kujenga miundombinu yenye ubora katika miradi yote inayoendelea na ile ambayo inatarajiwa kutekelezwa.

Ameongeza kuwa kutokana ongezeko la watu katika nchi zinazokuwa zinahitaji teknolojia za kisasa katika ujenzi wa miundombinu nchini ili ziweze kutosheleza mahitaji.

Mkutano huo umezikutanisha Taasisi za Wakala wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Wakala wa Majengo (TBA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Miundombinu ya Japani - Afrika (JAIDA)