Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUJENGA MADARAJA KUSIKOFIKIKA :BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga  kuhakikisha inajenga na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo yote yasiyofikika ili kusaidia wananchi kupata huduma za kijamii, kibiashara na uwekezaji.

Waziri Bashungwa amesema hayo mkoani Ruvuma Januari 26, 2024 wakati akifanya ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya barabara kutokea Songea Mjini hadi kufikia Wilaya ya Nyasa kupitia barabara ya Likuyufusi - Mtomoni (km 124) inayoenda kujengwa sehemu ya kwanza Likuyufusi - Mkayukayu (km 60) kwa kiwango cha lami pamoja na kukagua madaraja ya Mkenda na Mitomoni yatakapojengwa.

Kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo hayo, Waziri Bashungwa alilazimika kutumia takriban saa tano kwa kutumia usafiri wa miguu, mitumbwi na pikipiki maarufu kama boda boda hadi kufikia vijiji hivyo.

“Niwatake wasaidizi wangu, ninapokuwa katika ziara mikoani sitaki nikague barabara zilizojengwa kwa lami, nataka nikague maeneo ambayo hayana miundombinu ili Serikali ione namna ya kujipanga kutatua changamoto za wananchi”, amesisitiza Bashungwa.

Baada ya kukagua maeneo hayo, Waziri Bashungwa ametoa miezi miwili kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa daraja la zege katika eneo la Mitomoni ili wananchi wa maeneo hayo waondokane na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.

Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaunganishwa na barabara ya Unyoni Mpapa - Liparamba - Mkenda pamoja na barabara ya Likuyufusi - Mkenda kupitia Mto Ruvuma.

 

“Ujenzi wa Daraja hili utaunganisha Wilaya ya Nyasa na Mkenda na itaepusha njia ya mzunguko”, amefafanua Bashungwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nyasa, Eng. Stella Manyanya, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu cha kutokuwepo kwa miundombinu ya madaraja na kumuagiza Waziri wa Ujenzi kujionea changamoto hiyo ili hatua za ujenzi zianze.

Halikadhalika, Mkazi wa kijiji hicho Hadija Manyama, ameeleza kuwa wanapata shida ya usafiri na usafirishaji wa mazao yao upande wa pili hadi kufikia kuuza kwa bei ya hasara kwa sababu hakuna daraja la kuvuka.