Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

PROF. MBARAWA AKAGUA UJENZI WA SGR ISAKA-MWANZA


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR sehemu ya Isaka-Mwanza KM 341na kuwataka wakazi wa kanda ya ziwa kujipanga kutumia fursa hiyo ya uchumi.

Amesema wakati ujenzi wa SGR ukiendelea ni wakati wa wadau mbalimbali kubuni fursa za kibiashara na kihuduma zitakazoendana na matumizi ya treni mpya ya kisasa.

“Fursa za reli ni nyingi hivyo hakikisheni mnaziibua ili kuwezesha huduma ya treni itakapoanza kufayakazi kwa tija”, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha amewataka wafanyakazi wa reli hiyo kuwa  wazalendo kwa kuepuka tabia za wizi kwani tabia hizo zinaweza kuchelewesha mradi na kuleta hasara kwa Serikali na Mkandarasi.

Amesema ujenzi wa barabara za lami, meli katika ziwa Victoria, reli ya kisasa (SGR) na uboreshaji wa uwanja wa ndege ni dhamira ya Serikali kuunganisha mikoa na nchi jirani kwa usafiri wa njia zote hivyo ni vema kwa watanzania kujivunia miradi hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw, Adam Malima amemshukuru Waziri Mbarawa kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa miradi ya miundombinu mkoani humo na kumuahidi kuboresha huduma za ulinzi na usalama kwenye miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.

“Mheshimiwa Waziri sisi Mwanza tunajengewa daraja la Kigongo –Busisi, meli za kutoa huduma ukanda wote wa ziwa Victoria, jengo la abiria katika uwanja wa ndege na SGR ndio itapita juu hapa mjini tunafarijika sana kwa kweli”, amesema Mkuu wa mkoa Malima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw, Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa sehemu ya tano ya SGR umefikia asilimia 23.4 na kumhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wataendelea kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili kazi ikamilike kwa wakati na ubora unaokusudiwa