Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

PELEKENI VIJANA KUJIFUNZA UFUNDI STADI


Wito umetolewa kwa wazazi, walezi na wafadhili kuwapeleka vijana wao kupatiwa mafunzo ya ufundi stadi hususan vijana wa kike ili kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.

Wito huo umetolewa mkoani Morogoro katika mahafali ya 25 ya wanachuo wa mafunzo ya ufundi stadi katika Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) na Mkurugenzi Msaidizi wa Barabara Sehemu ya Barabara Kuu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Lightness Chobya.

"Nitoe wito kwa wazazi na walezi wa vijana wetu tuwekeze katika kuwasomesha ufundi stadi, hatutapoteza kitu na elimu hii itakuwa mkombozi kwa vijana wetu na wataweza kujiajiri wenyewe na kujiiinua kiuchumi na familia kwa ujumla", amesisitiza Eng. Chobya.

Eng. Chobya, amewasihi wahitimu hao kuendelea kuwa wadadisi, wabunifu na wenye uthubutu wa kufanya mafunzo kwa vitendo pamoja na kujiendeleza zaidi wakizingatia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ili kuwa mafundi wazuri huko mbeleni na kulisaidia Taifa kutoka na ujuzi walioupata.

Aidha, ametoa wito kwa Taasisi za Serikali na binafsi kufungua macho na kuwaona wanafunzi wanaomaliza mafunzo katika taasisi hiyo hususan katika suala la ajira ili kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Eng. Chobya ametoa rai kwa taasisi hiyo kuendelea kuitangaza Taasisi kwa njia mbalimbali ili iweze kufahamika vizuri zaidi kwa watanzania na wadau mbalimbali pamoja na kuzitangaza shughuli nyingine zinazoendana na mafunzo.

 Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo Eng. Mahmoud Chamle, ameeleza kuwa katika awamu ya 25 ya wahitimu wa mafunzo ya ufundi kwa mfumo wa CBA (Comptence Based Assessment) ulioanzishwa mwaka 2013 ni 174 ambapo kati ya hao wavulana ni 142 na wasichana ni 32 katika fani 8

Mkuu wa Taasisi hiyo ametaja mafanikio wanayojivunia ikiwa ni pamoja na wahitimu wa taasisi hiyo waliohitimu miaka ya nyuma zaidi ya asilimia 90 wameajiriwa kwenye sekta rasmi na zile zisizo rasmi.

Pia Chamle ametaja kozi za muda mrefu zinazotolewa na Taasisi hiyo ambazo ni Stashahada (Diploma NTA Level 4, 5 na 6) katika fani za Uhandisi wa Umeme, Uhandisi Ujenzi na Uhandisi Umeme.

Pia inatoa mafunzo ya ufundi stadi (VET) katika fani za ufundi umeme wa magari, umeme wa majumbani, uchomeleaji vyuma, uashi, magari, bomba, barabara na matengenezo na uchoraji wa ramani za majengo.

Katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika mkakati wa kuondoa umaskini, Taasisi ya ICoT pamoja na fani za ufundi wahitimu walizozipata pia wamejifunza masomo mbalimbali yakiwemo ya ujasiriamali, kiingereza, mawasiliano, hisabati, sayansi uhandisi, stadi za maisha na michoro ya kifundi.

Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), ni moja ta Taasisi zilizo chini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) iliyoanzishwa kwa kuunganishwa kwa vyuo vya Ujenzi -  Morogoro (MWTI) na Chuo cha Teknolojia Stahiki ya NguvuKazi (ATTI), kilichopo mkoani Mbeya na kusajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET).