Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

PAC YARIDHISHWA UJENZI WA BARABARA NJOMBE-MORONGA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeelezea kuridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa barabara mkoani Njombe.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Japhet Hasunga amesema baada ya kupitia na kukagua barabara ya Njombe-Moronga KM 53.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika wameridhika na utekelezaji wa mradi huo.

“ Nitoe wito kwa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani na maelekezo mengine halali ili kuepusha ajali na kuwezesha barabara  kudumu kwa muda uliokusudiwa”, amesema Mhe. Hasunga.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutoa fedha zaidi ya bilioni 5 ili kuwezesha kujengwa kwa barabra kuelekea eneo la Liganga na Mchuchuma na kusema hatua hiyo itawezesha uwekekezaji mkubwa wa chuma na makaa ya mawe na hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo.

“ Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara za lami za kimkakati hali itakayovutia wawekezaji wa kilimo, utalii na viwanda mkoani humu”, amesema Mtaka.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi, Eng. Aisha Amour ameishukuru kamati ya PAC na kuahidi Wizara itatekeleza maelekezo yake ili kuboresha miradi inayoendelea na hivyo kuleta tija kwa wakati.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iko mkoani Njombe kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo pamoja na mambo mengine imekagua barabara ya Njombe-Moronga KM 53.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.