Habari
"ONGEZENI KASI UJENZI WA BRT 3" KAKOSO

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezungumzia umuhimu wa Serikali kumsimamia kikamilifu mkandarasi SINOHYDRO Corporation Ltd anayejenga Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT3) ili ukamilike kwa wakati.
Akizungumza leo Machi 17,2025 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Moshi Kakoso amesema mradi huo unaoanzia katikati ya jiji la Dar es salaam hadi Gongolamboto Km 23.3 ukikamilika utapunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi.
"Serikali imewekeza fedha nyingi katika barabara za BRT zilizozunguka jiji la Dar es Salaam hivyo hakikisheni zinakamilika na tija inaonekana kwa kupunguza msongamano na kuwawezesha wananchi kufika katika maeneo yao ya kazi na biashara kwa wakati.
"Tumejiridhisha na kasi inayoenda lakini tuna mashaka muda uliopangwa kumalizika kwa mradi huu umebaki miezi minne hivyo fanyeni kazi usiku na mchana ili aweze kukabidhi mapema", amesema Kakosa.
Mwenyekiti Kakoso ameshauri Serikali kuangalia sanifu za miradi ya barabara za BRT ili ziwe wezeshi pindi magari yanapopata dharula.
"Tunashauri watalaamu kuangalia maeneo ambayo hayana ulazima kuweka kingo wazipunguze au kutoa kwaajili ya kujenga mazingira rafiki ambayo yatasaidia miundombinu hii kuwapa fursa nzuri wananchi wanufaike nayo", amesisitiza Kakoso.
.Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema mradi wa BRT 3 umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wanaofanya biashara wakati ujenzi wa mradi huo unaendelea kuacha mara moja kwani licha ya kukwamisha kazi pia ni hatari kwa maisha yao.
"Namwagiza Mkandarasi aongeze mafundi, vibarua ili kukamilisha mradi huu ifikapo mwezi Juni", amesema Kasekenya.
Meneja wa Mradi wa BRT3, Mhandisi, Frank Mbilinyi amesema BRT kwa kushirikiana na Serikali za mitaa na ustawi wa jamii wanaendelea kuwapa elimu wananchi ili kuacha kuvamia maeneo ambayo ni ya barabara na ujenzi unaendelea.
Serikali inaendelea kujenga barabara za kupunguza msongamano jijini Dar es salaam ambapo awamu ya kwanza Kivukoni-Kimara- Magomeni -Moroccco km 20.9 na awamu ya pili Magomeni- Mbagala imekamilika.
Awamu ya tatu Posta-Gongolambotokm 23.3 na awamu ya nne katikati ya jiji - Tegeta km 29.13 ujenzi wake unaendelea.